Unamkumbuka selemani mathew?

08Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Unamkumbuka selemani mathew?
  • M/kiti Chadema Kusini aanika
  • Apiga debe ‘shime tujiandikishe’
  • mwelekeo wao joto la uchaguzi

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekuja na mkakati unaolenga kuwapata viongozi bora wa kukiwakilisha, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Suleman Mathew (katikati), akizungumza katika mkutano wa chama hicho juzi mjini Mtwara.

Mkakati huo unatajwa na Mwenyekiti wa Chadema wa kanda hiyo, Seleman Mathew, ni wa kuwataka wanachama wenye nia ya kuwania uongozi katika uchaguzi huo kujitokeza mapema, ili wapimwe utendaji wao.

"Yaani ni kwamba, chama kinawataka wajitokeze mapema wapimwe utendaji wao katika maeneo wanayotoka, ili kuona kama wanafaa kuteuliwa na kukiwakilisha chama hicho, katika uchaguzi mkuu," anasema Mathew.

Mwenyekiti, aliyewahi kuwa mwanasoka nafasi ya ulinzi kwa vilabu vya Yanga na Tukuyu Star, anasema, wanachama hao ni wale wa ndani na nje ya kanda, ambao wana nia ya kuwania udiwani, ubunge ukiwamo wa viti maalum na hata urais mwaka huu.

"Wajitokeze mapema ili tujiandae mapema kwa ajili ya uchaguzi mkuu, mwaka huu 2020 ni uchaguzi mkuu na katika kanda yetu, tuna jumla ya kata 515 na majimbo 27 ya uchaguzi," anasema.

Mathew anafafanua kwamba, kanda hiyo inajumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na kwamba viongozi wamekutana na kujadili jambo hilo na kuamua kuwaomba wanachama wanaotaka kuwania uongozi wajitokeze mapema.

Anasema, suala la kuwapima wanachama wao mapema ni la msingi kwa maendeleo ya chama hicho na kwamba ni muhimu kwa wenye nia ya kujitosa kinyang’anyiro; cha uongozi, wakazingatia hilo.

UTARATIBU

Mathew anataja utaratibu wa kugombea uongozi kwamba, mwanachama anayetaka udiwani, anatakiwa kuwasilisha kusudio lake kwa maandishi katika ofisi za chama katika kata husika na nakala kupelekwa wilayani, ambayo iko kata anayotaka.

"Anayetaka kugombea ubunge, awasilishe kusudio lake la kuwania kwa katibu mkuu kupitia kwa katibu wa kanda na nakala ya kusudio hilo awasilishe kwa katibu wa mkoa, ambao jimbo analotaka kugombea limo na kwa katibu wa jimbo husika analotaka kugombea," anasema.

Anasema, anayetaka kugombea urais anatakiwa kuwasilisha kusudi la kugombea kwa katibu mkuu, hivyo wanachama wote wenye sifa wanakaribishwa kutangaza kusudio la kugombea nafasi hizo.

"Tunatoa wito kwa wanachama wote walioko ndani na nje ya kanda yetu wenye nia ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge ukiwamo wa viti maalum na urais, wajitokeze sasa ili wapimwe utendaji wao mapema katika maeneo wanayogombea," anasema.

DAFTARI LA KURA

Mathew anasema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imekuwa ikiboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali nchini, ili kupata taarifa sahihi za wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

“Awamu ya hili linafanyika katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na Visiwa vya Unguja na Pemba. Tumefuatilia kwa ukaribu zoezi hili, lakini kwa bahati mbaya sana haliendi kama vile inavyotarajiwa.

"Tunataka wananchi wa Kanda ya Kusini na maeneo mengine wapate haki yao ya kujiandikisha na baadaye wapate fursa ya kupigakura kuwachagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi mkuu," anasema.

Mathew anarejea Sheria ya Uchaguzi, kwamba inaruhusu daftari hilo kuboreshwa mara mbili kwa kipindi cha miaka mitano, hata hivyo anadai bado kasi haimridhishi.

"Kwa sasa uboreshaji huo unafanyika kwa kipindi kifupi sana cha siku saba, ambacho tunaona uboreshaji huu hautakuwa na mafanikio makubwa kwa sababu vyama vya siasa vimezuiwa kufanya siasa kwa takriban miaka minne sasa. Hivyo, hamasa kwa wananchi itakuwa ndogo," anasema.

Mwenyekiti huyo anawahimiza viongozi wa ngazi mbalimbali katika kanda na wanachama, kuhamasishana kwenye vitongoji na matawi, umma kwenda kujiandikisha katika daftari hilo.

Anasihi uhamasishaji usiwe kwa wanachama tu, bali hata wananchi wengine katika maeneo yao, ili nao waende kujiandikisha na hatimaye wapate haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Anarejea taraifa alizo nazo akidai, uandikishaji kwa maeneo yote ya mkoa wa Lindi na Mtwara, utaanza Januari 12 hadi 18 mwaka huu na anafafanua:

"Kwa ratiba hiyo, ninawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi ili mpate haki yenu ya kuchagua viongozi mtakaowataka katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu."

KUSINI & RASILIMALI

Mwenyekiti huyo anasema, ukanda wa Kusini una rasilimali nyingi, ikiwamo gesi, makaa ya mawe, mazao ya bahari, korosho, kahawa, ufuta, mahindi, maharage, mbaazi, choroko.

Anasema, utajiri wa rasilimali hizo zinaweza kuwanufaisha wananchi wa Kusini na kukuza uchumi wao kwa jumla, jambo analoamini chama chake kikiingia madarakani, itahakikisha wahusika wananufaika na rasilimali zao.

Anataja mazao ya choroko na mbaazi bado yamekuwa na bei ndogo sana na wakati mwingine kukosa kabisa wateja, jambo analolalamika kuna pengo la uratibu kibiashara.

"Chadema tunaamini katika utawala wa majimbo, hivyo Kusini kama moja ya jimbo (province) baada ya ushindi katika uchaguzi mkuu, tutahakikisha suala matumizi ya rasilimali za kusini kupaumbele ni Kusini kwanza," anasema.

Anasema, utawala wa Jimbo la Kusini ndiyo utakaokuwa na wajibu mkubwa wa kusimamia rasilimali za Kusini, kwa kuwatafuta wawekezaji na masoko ya mazao ya wakulima wa huko.

"Tunaunga mkono pia maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama John Mnyika ya kutekeleza na kusimamia vipaumbele vitano vya chama kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu," anasema.

Mathew anavitaja vipaumbele hivyo, kuwa ni: Kudai tume huru ya uchaguzi; kuendeleza Chadema ni msingi; maandalizi ya wagombea; Chadema ‘digital’; na ilani ya uchaguzi.

Habari Kubwa