Bobi Wine sasa ‘ingizo jipya’ kumkabili Museveni 2021

08Jan 2020
Mashaka Mgeta
Nipashe
Bobi Wine sasa ‘ingizo jipya’ kumkabili Museveni 2021

IIMEKUWA kawaida katika Uchaguzi Mkuu wa Uganda kuwashuhudia washindani wawili wakongwe, Rais Yoweri Museveni wa National Resistance Movement (NRM), kupata ushindani wa karibu kutoka kwa Kizza Besyige wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC).

Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, katika nyendo zake za kisiasa. PICHA: MTANDAO.

Hali hiyo ilijitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Uganda uliofanyika kwa nyakati tofauti katika miaka ya 2001, 2006, 2011 na 2016. Mara zote hizo, Rais Museveni ameibuka na ushindi na kuendelea kutawala tangu alipoingia madarakani Januari 26, 1986.

Lakini, uchaguzi mkuu wa mwakani nchini humo, unatarajiwa kupata ‘ingizo jipya’ la Mbunge wa Kyaddondo Mashariki, wilayani Wakiso katika mkoa wa Kati, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.

Mbunge huyo ambaye ni msanii wa muziki wa pop, ameshatangaza nia hiyo, ingawa kwa kuandamwa na ‘kash kash’ nyingi za kisiasa.

Mwanasiasa huyo aliyezaliwa takribani miaka minne kabla ya Museveni kuingia madarakani, mara ya kwanza, hivi sasa akiwa na miaka 37, wakati Rais huyo aliyedumu madarakani kwa muda mrefu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikikaribia siku chache kuingia mwaka wa 34 sasa.

Bobi Wine anayejulikana pia kwa jina la utani la ‘Rais wa Ghetto’ ni mkosoaji mkubwa wa Rais Museveni anayeungwa mkono na Waganda wengi hususani kundi la vijana.

Bobi Wine aliwekwa ndani kutokana na madai ya kushiriki tukio la kupigwa mawe kwa msafara wa Rais Museveni. Alikana kuhusika katika tuhuma hizo na akaachiwa kwa dhamana.

"Kwa niaba ya watu wa Uganda, nitashindana na wewe (Museveni) katika uchaguzi mkuu ulio huru na haki mwaka 2021," Bobi Wine, alinukuliwa kutamka hayo jijini Kampala.

"Ninajua hatari ninayokwenda kukutana nayo kukabiliana na Museveni, lakini nimepewa nguvu na ushawishi mkubwa na Waganda wanaoniona mimi ndiye kiongozi ninayewafaa,” amekaririwa na shirika la habari la AFP.

Bobi Wine anajinasibu kuwa mtetezi wa watu maskini na kielelezo cha haki na demokrasia kwenye jamii.

Bunge la Uganda, liliondoa kifungu kinachoweka ukomo wa mtu anayetaka kugombea urais nchini humo kuwa na miaka isiyozidi 75, hali ambayo ilifungua milango kwa Museveni aliyezaliwa Agosti 15, 1944 kuwa mnufaika mkuu wa hatua hiyo, hivyo kugombea tena kwa mara ya sita.

Wanaomuunga mkono Rais Museveni katika kuwania kwake urais wanasema, kiongozi huyo anapaswa kubaki madarakani kwa maslahi ya utulivu na maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo.

Badahi ya vyombo vya habari vilihamisha tafsiri ya siasa hizo kuwa vijana wa Uganda, wana utashi na Bobi Wine na ndio sehemu kubwa ya wananchi.

ATAWEZA?

Kuna swali gumu linaloibuka kwamba, bado hajaweka mpango mpana wa namna atakavyoshughulikia kero sugu zinazoikabili nchi hiyo na watu wake, hasa ukosefu wa ajira na huduma duni za afya na elimu.

Bobi Wine anatamba kuwa, yeye ni kiongozi na kwamba Uganda ina wataalamu na wanataaluma wengi wanaoweza kushughulikia masuala ya kitaalamu.

Kwa upande wake, Rais Museveni amekuwa anaishusha thamani hoja hizo akimuita ni ‘msanii wa nyimbo kwenye klabu za usiku.’ Lakini, katika kipindi cha takribani miezi 18 kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa 2021, amekuwa akizungunguka nchi nzima akitoa pesa kwa makundi maalum ya kijamii, ikiwa sehemu ya operesheni ya kukuza utajiri wao.

Pamoja na kujiongezea umaarufu kwa Waganda na nje ya taifa hilo lililo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bobi Wine, anaendelea kupata misukosuko kisiasa ikiwamo kukamatwa na polisi mara kadhaa.

Kamanda wa Polisi mwenye dhamana ya operesheni, kwenye Kituo cha Polisi cha Kasangati, Supritendat Msaidizi (ASP) Andrew Angume, alijeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya vyombo vya dola na wananchi (wanaomuunga Bobi Wine) kwenye Halmashauri ya Mji wa Kasangati.

ASP Angume, aliongoza timu ya askari kumkamata Bobi Wine na wanachama wengine wa vuguvugu la ‘nguvu ya umma’ walipokuwa kwenye mkutano unaohusu azma ya mwanasiasa huyo kuwania urais 2021.

Polisi walimshutumu Bobi Wine pamoja na Mbunge wa Manispaa ya Bugiri, Asumani Basalirwa na mwenzao wa Kawempe Kaskazini, Latif Ssebagala, kwamba waliitisha mkutano wa mashauriano hayo kinyume cha sheria za nchi hiyo.

Baada ya kuwakamata wabunge hao, walipelekwa kwenye Kituo cha Polisi cha Kasangati, wilayani Wakiso aliloshikiliwa kwa muda kasha alihamishiwa kwenye Kituo cha polisi Nagalama, wilayani Mukono.

Hata hivyo, ghasia zilizuka kati ya wafuasi wa ‘nguvu ya umma’ na polisi kiasi cha kusababisha wana-usalama hao kufyatua risasi na mabomu ya machozi kuwatawanya.

ASP Angumea alijeruhiwa kwa bomu la machozi lililorushwa na askari mwenzake, likiwalenga ‘nguvu ya umma’.

Naibu Msemaji wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kampala, Luke Owoyesigyire, alithibitisha kujeruhiwa kwa ASP Angume, pasipo ufafanuzi wa kinai.

Mapambano hayo yalitokea, baada ya kutanguliwa na tukio alilopanga kulifanya jimboni mwake, lakini ‘likazimwa’ na askari polisi waliofika mapema kwenye eneo la tukio na kuwasambaratisha.Waandamanaji walichoma matairi ya magari na kufunga barabara wakati polisi wakisaidiwa na magari ya kiaskari.

Polisi ilisema wanasiasa hai hawapaswi kufanya mkutano wa hadhara, inayolenga kusaka ‘makubaliano mbele ya umma.’

“Mkutano unapaswa kufanyika sehemu ya ndani kama inavyoelekezwa na Tume ya Uchaguzi,” anatamka msemaji wa polisi, Enanga, alipozungumza na waandishi wa habari.

Bobi Wine, aliwahi pia kukamatwa mara kadhaa alipofanya tamasha la muziki akiwa mbunge, katika matukio ambayo alipigwa marufuku tangu mwaka 2017.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Uganda, mgombea urais mtarajiwa anapaswa kufanya mashauriano ya kutaka kuungwa mkono nchi nzima katika kipindi cha miezi 12, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu. 

Mwisho

 

Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, katika nyendo zake za kisiasa. PICHA: MTANDAO.

Habari Kubwa