Jicho urais marekani…

08Jan 2020
Ani Jozen
Nipashe
Jicho urais marekani…
  • Uchaguzi 2020 watangaza nia urais Democratic wapukutika?
  • Chasakwa kigingi kumng’oa Trump

WACHAMBUZI wa habari wamekuwa na kazi ya ziada hivi karibuni nchini Marekani, kuangalia mazingira ya kusitisha mbio za kutafuta kupewa bendera ya chama cha Democratic, kwa uchaguzi wa rais nchini huko baadaye mwaka huu.

Moja ya sababu za mahangaiko hayo ni kuwa aliyeng’atuka katika mbio hizo, Julian Castro, alikuwa mtangaza nia pekee aliyebakia kwenye kundi hilo ambaye ni mzaliwa wa jamii ya ki-Hispania, wanaotokea Amerika ya Kusini kwa kuzaliwa.

Ili mtu aweze kugombea urais nchini Marekani, inabidi awe amezaliwa nchini humo, lakini kwa kawaida mizizi haiondolewi machoni.

Moja ya sababu za jambo hilo kuleta sokomoko au kujitafuta kwa kiasi fulani, ni hisia miongoni mwa wananchi wengi nchini humo wenye asili ya Kihispania kuwa itafika wakati nao watapata kiongozi anayeweza kuungwa mkono kugombea urais.

Inajulikana, kama ilivyo kwa watu wenye asili ya Afrika wenye asili ya Amerika ya Kusini, pia wanategemea chama cha Democratic, ndiko anakoweza kuibuka mtangaza nia mwenye uwezo na kukubalika na siyo chama cha Republican. Ina maana, hakuna uwezekano mwanasiasa kutoka jamii hiyo kujitokeza kuinua matumaini yao 2020.

Mwanasiasa huyo alikuwa Waziri wa Nyumba katika zama za Rais Barack Obama, pia alikuwa Meya wa Jiji la San Antonio, jimbo la Texas na hadi aking’atuka mbio hizo hapakuwa na mtangaza nia mwingine anayetokea jamii hiyo aliyethubutu kujipambanua.

Alianza kampeni yake na kuisogeza mbele kwa kuelezea nia ya kutaka nchi ya Marekani, iwe ni taifa ambalo kila mwananchi ana umuhimu ambako kila mmoja anaweza kupata kazi nzuri, kuangaliwa afya na mahali panapofaa kuishi.

Wachambuzi wa habari wanasema, alipokuwa katika kinyang’anyiro hicho alikuwa kielelezo kwa utungaji sera kuhusu uhamiaji na kupambana na umaskini na kwa maana hiyo, unaweza kusema hata nchi za Afrika zimepoteza rafiki.

Katika ufafanuzi wao, wanasema kuwa Casto (mwenye umri wa miaka 45 ni mpenda siasa za kimaendeleo, ambao nchini Marekani wanaitwa ‘waliberali’ wakati barani Ulaya wanaitwa ‘progressives’ jambo ambalo ni kama kitu kilichosahauliwa na magazeti, redio na televisheni wakati wa kampeni yake.

Licha ya kuinua hisia kali wakati wa kampeni miongozi mwa wafuasi wa chama hicho katika majimbo tofauti, hakufaulu kuingia katika anga za watangaza nia watano wa juu, au kuwa gumzo miongoni mwa wafuasi wa chama hicho na jamii kwa jumla.

Kuondoka kwake ni hatua nyingine ya kupungua idadi ya watangaza nia kutoka jamii mbalimbali za taifa la Marekani na kuainisha ugumu kwa kurudia alichofanya Barack Obama, aliposhinda kinyang’anyiro cha kupata mgombea Democratic na kushinda uchaguzi wa 2008.

Akitoa waraka wa video kujionoa katika kinyang’anyiro hicho, mwanasiasa huyo alisema amefikia tamati kuwa ni wazi kwamba wakati haujafika kwake yeye au mtu kama yeye kuwa na umuhimu katika kinyang’anyiro hicho.

Alikuwa kwenye kampeni hiyo kwa mwaka mzima ambako alitembelea maeneo ya mpakani na makazi ya watu wasio na nyumba, akaona kiwango cha kutokuwa na shauku na kampeni yake miongoni mwa vyombo vya habari na wapigakura, akabwaga manyanga.

Alisema bado yuko katika harakati, licha ya kutosema kuwa baada ya kuondoka katika kampeni hiyo, anataka kufanya nini, hasa katika siasa akiainisha dhamira yake ya kuendelea na kampeni ya haki za msingi kwa wote.

Moja ya maeneo ambayo Castro aliyafanyia kazi wakati akiwa katika kampeni ni mauaji holela ya raia wa Marekani wenye asili ya Afrika au ya Amerika ya Kusini, tatizo ambalo limezidi kukua miaka ya karibuni.

Wakati Rais Obama alipokuwa madarakani, polisi katika miji au jiji mbalimbali ya Marekani, walikuwa na tabia ya kutumia kisingizio chochote kupiga risasi badala ya kumkamata mtu ili kumhoji, endapo ana asili ya Afrika. Alipoingia madarakani Rais Donald Trump, raia kutoka kusini ndiyo taabu.

Inatajwa pia kuwa Castro alikuwa anafikiriwa na aliyekuwa mgombea wa urais wa chama hicho mwaka 2016, Hillary Clinton ambaye alishindwa katika uchaguzi na Trump, kuwa Castro angeweza kuwa mgombea mwenza wake.

Moja ya michango yake iliyoleta mijadala katika chama hicho na kwingineko Marekani ni wazo lake kuwa wanaovuka mpaka bila vyeti vya kusafiria (hasa kutoka Mexico) wasitajwe kama wahalifu.

Inasemekana alichosema kulianza kuwa mtego kwa wagombea wengine wa chama hicho ambacho wapigakura wake wengi wanatoka katika jamii ya ki-Hispania, na baadhi wakakubaliana naye.

Castro alipokuwa Meya wa San Antonio, alianzisha mpango wa kupeleka watoto malezi kabla ya shule, prekindergarten, yaani wakiwa wadogo kabisa kuwezesha mama vijana wafanye kazi wajiendeleze kimaisha, kwani Marekani si rahisi kulipa mtu kusaidia malezi.

Alitoa hotuba katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho mwaka 2012 ambayo ilimwinua katika ngazi za siasa kitaifa, akitoa orodha ya mapendekezo kuhusu maeneo kama nyumba, elimu, usimamizi wa kesi za jinai, uchumi na kuainisha wapi mfumo wa usimamizi wa kazi za polisi unaweza kuboreshwa.

Castro alionyesha pia dhamira ya kulinda maeneo yanayokaliwa na watu wenye utamaduni wa asili, kulinda hifadhi za wanyama na hata wanaofugwa na kupunguza kwa kiasi kikubwa sumu inayotokana na risasi inayoingia katika maji.

Alitoa pendekezo la kuongeza kodi kwa mali za kurithi hasa wale wanaorithi mamilioni ya fedha Dola za Marekani, akijaribu kuandaa mpango wa kuondoa umaskini, kufuta kabisa hali ya kukosa chakula ambayo ilipanua kufahamika kwake kwa matabaka ya chini kabisa.

Hakuweza kuungwa mkono na matabaka ya kati, na licha ya kufaulu kuingiza kiasi cha dola laki nane za michango ya kuendeleza kampeni yake, hakupata viwango vya kuridhisha vya kukubalika kwa wapiga kura katika kura za maoni za hapa na pale kuhusiana na kampeni wa watangaza nia Democratic.

Alishiriki mijadala minne ya kwanza ya watangaza nia, lakini hakupata viwango vya kukubalika kwa wapigakura kuendelea nazo.

Habari Kubwa