RC aagiza tathmini mishahara watumishi

08Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
SINGIDA
Nipashe
RC aagiza tathmini mishahara watumishi

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, amesema kila mtumishi wa serikali katika mkoa wake kuanzia mwaka huu atatakiwa kuonyesha mafanikio yanayotokana na mishahara anayolipwa na serikali kupitia kaulimbiu maalum iliyoandaliwa na mkoa ya “mshahara wangu upo wapi”.

Amesema tathmini hiyo itafanyaka mwisho wa mwaka huu, huku akionya watumishi kuhusu kujihusisha na mambo ya siasa, badala yake kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za serikali.

Akizungumza na watumishi wa mmma wa mkoa wa Singida katika mkutano maalum wa kwanza katika mwaka huu mjini Singida jana, Dk. Nchimbi alisema mkoa umeamua kuiishi kaulimbiu hiyo baada ya kuona mafanikio ya kupigiwa mfano yaliyopatikana kutoka kwa wanufaika wa mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Alisema katika mpango huo, ruzuku ya Sh. 20,000 ilitolewa kwenye kila kaya yenye sifa katika halmashauri sita kati ya saba za mkoa pamoja na fedha za masharti ya afya na elimu ambazo kila kaya yenye mtoto anayesoma shule ya msingi na sekondari na wale chini ya miaka tano, ilipewa kuanzia Sh. 2,000 hadi 6,000.

Alisema ruzuku hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa kaya maskini katika kuwanunulia sare, madaftari na kulipia matibabu hasa kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (NHIF).

Aliongeza kuwa hadi kufikia Januari mwaka huu, jumla ya kaya 38,136 kutoka katika vijiji 278 zimenufaika na ruzuku hiyo na jumla ya Sh. 37.9 ziliwafikia walengwa.

“Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna kipindi ambacho watumishi wa umma watakuwa na maisha bora kama hiki cha serikali ya awamu ya tano, imeshaboresha kwenye kila sekta kama miundombinu, huduma za afya na elimu, itashindwaje kuboresha maisha ya watumishi umma?" Alihoji.

Dk. Nchimbi alisisitiza kuwa watumishi wazembe hawatavuka mwaka 2020 bila kuondolewa mara moja kupisha watumishi wanaoendana na kaulimbiu ya 'Hapa Kazi Tu'.

Alisema mbali na kuhakikisha kuwa mishashara ya watumishi inaleta tija kwenye familia na kuboresha uchumi, tayari mkoa unatekeleza mikakati mahsusi ya kilimo cha kisasa cha pamoja cha zao la korosho kwa wananchi wake.

Alitoa rai kwa watumishi na wananchi kujitokeza ili kupatiwa maeneo hayo ili kuyaendeleza kwa pamoja.

“Hadi sasa, Singida siyo maskini, kame wala yenye njaa kama iliyokuwa ikitafsiriwa na baadhi ya watu hapo awali. Tayari hekta 12,000 za kilimo cha pamoja (block farming), zimepandwa mikorosho na zimeanza kuzaa korosho katika Wilaya ya Manyoni.

"Ninatoa shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutupatia pikipiki 10 ili ziweze kusaidia katika kazi hii," alisifu.

Alisema utafiti uliofanyika hivi karibuni, umeonyesha ardhi ya mkoa huo ina ubora mkubwa wa kustawisha zao la korosho kwa muda mfupi kulinganisha na maeneo mengi nchini, hivyo hakuna sababu watumishi na wananchi kutochangamkia fursa hiyo adimu.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa, ambaye yuko mkoani Singida kwa ziara ya kikazi ya siku nne kuazia jana, alitoa wito kwa waajiri na watumishi wa umma kuwasilisha taarifa sahihi kwa wakati kwenye ofisi yake ili zifanyiwe kazi katika kipindi kilichopangwa.

Alisema tatizo na vikwazo vingi vya watumishi kama malimbikizo ya mshahara, kulipwa mafao, kupanda madaraja, uhamisho na mafunzo vinatokana na uwasilishaji taarifa na kutozingatia muda sahihi wa kufanya hivyo.

Aliwataka maofisa utumishi kutokujifanya miungu watu na badala yake watimize wajibu wao wa kufanya kazi zao kwa weledi.

Habari Kubwa