Kigogo Chadema atishia kujiuzulu

08Jan 2020
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Kigogo Chadema atishia kujiuzulu

KIGOGO mmoja wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, ametishia kujiuzulu wadhifa wake, ikiwa kamati kuu ya chama hicho itarudisha majina ya wagombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambao hawakufanya kazi majimboni, akiwaita ni virusi.

Aliyeapa kutokubaliana na wagombea ubunge walioshindwa kutekeleza sera ya Chadema ni Msingi majimboni mwao ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila.

Kilawila alitangaza vita hiyo jana mjini Moshi, wakati akifungua kikao kazi cha kimkakati cha Baraza la Wanawake Mkoa wa Kilimanjaro (Bawacha), ulioitishwa na Mbunge na Mjumbe wa Kamati Kuu, Grace Kiwelu.

“Sasa tunapojiandaa kwenda kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, kila mtu kwenye mkoa huu atakula alikopeleka mboga. Sijui kama mnanielewa, yaani wewe unataka kuwa mbunge utatuonyesha kazi uliyofanya, niko tayari kujiuzulu nafasi yangu ya mkoa kuliko kuletewa virusi ambavyo havikufanya kazi.

“Tumeelewana eeh, yaani wewe mwenzako akaanzishe Chadema ni Msingi, akalale nje ya ndoa yake siku tatu, nne au mwezi, halafu mtu mwingine aje na senti zake kwa sababu tu amebarikiwa kuwa na senti, anataka umwidhinishe kuwa mgombea wa nafasi fulani ndani ya chama.

“Hiyo haitakaa itokee na Mungu apitishe mbali. Sasa hivi sitaangalia sura na bahati mbaya au nzuri, niwaambie katiba yetu imebadilishwa, yaani muziki unaanzia hapo. Katiba yetu imebadilishwa na sio kule wanapitisha tena (kamati kuu) ni hapa hapa mkoani, tunanyoana hapa hapa.”

Katika hotuba yake Kilawila aliwaeleza wajumbe hao wa Bawacha kuwa: “Hatutakuja kusema ooh fulani kaja katoka Marekani na ana hela, hizo hela zinamsaidia yeye, wanyonge wetu na uji wetu tutaendelea kubaki hapa, tumeelewana eeh. Kwa hiyo kafanyeni kazi, niwaombeni sana hilo mkalizingatie.”

Alieleza kuwa katika watu wanaofanya vizuri sasa hivi ni Baraza la Wanawake wa Chadema na wanakwenda kwa spidi kubwa, lakini mabaraza mengine yamebaki nyuma, ingawa ana hakika kwa spidi hiyo na mikutano ya wanawake inayofanyika inakwenda kuamsha ari.

Kutokana na mwelekeo huo, Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa kuanzia Januari 22 mwaka huu Baraza la Uongozi la Mkoa linaanza ziara Jimbo la Same Mashariki.

“Tunakuja huko tuweke mikakati pamoja na somo litakalotolewa hapa leo, lakini tuweke mikakati ya pamoja ni namna gani tunakwenda. Tukitoka Same Mashariki, tutakuja Same Magharibi, tutakuja Mwanga, tutakwenda Rombo na tutakuja Vunjo, tutakuja Moshi Vijijini, Moshi Mjini, tutakwenda Hai na tutamalizia na Siha,” alieleza Kilawila.

Awali, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Kilimanjaro na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Grace Kiwelu, akitoa hotuba yake kuhusu mwelekeo wa mwaka wa uchaguzi (2020) kwa Baraza la Wanawake, alisema katika kufikia malengo ya ushindi ya Chadema, Bawacha Kilimanjaro itaboresha zoezi la Chadema ni msingi na kuhamasisha wanawake wengi kujisajili katika daftari la chama hicho.

“Tunataka kuwainua wanawake kwa kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi ili kufikia azma ya kauli mbiu yetu ya maendeleo ni mwanamke. Tutaratibu mafunzo ya uongozi kwa wanawake na kuhamasisha wanawake wengi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” alisema Kiwelu.

Habari Kubwa