Katwila amulika rekodi kubwa Mapinduzi Cup

08Jan 2020
Isaac Kijoti
ZANZIBAR
Nipashe
Katwila amulika rekodi kubwa Mapinduzi Cup

HUKU timu yake ikifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amesema anataka kuandika rekodi ya kulitwaa kombe la michuano hiyo, kwa mara ya pili akiwa kocha baada ya kufanya hivyo wakati akiwa mchezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari kisiwani hapa, Katwila alisema amefurahi kuona Mtibwa Sugar imepata nafasi ya kushiriki michuano hiyo mwaka huu, baada ya kutoshirikishwa kwa muda sasa.

Katwila alisema mara ya kwanza kwake kushiriki michuano hiyo alikuwa mchezaji na walifanikiwa kulibeba kombe hilo, jambo ambalo atafurahi kama atalitwaa akiwa kocha.

"Hii ni mara yangu ya pili kuja hapa (Pemba), mara ya kwanza nilikuja kama mchezaji na tulitwaa ubingwa nitafurahi kuubeba sasa nikiwa kocha," alisema.

Juzi Mtibwa Sugar ilifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuitoa Chipukizi kwa mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia mechi kumalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, Chipukizi ilikuwa ya kwanza kuliona lango la Mtibwa dakika ya tano kupitia kwa Suleiman Nassor.

Mtibwa ilibidi kusubiri hadi dakika ya 63 kabla ya Haroun Chanongo kuisawazishia na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ndipo changamoto ya mikwaju ya penalti ilipochukua nafasi yake.

Katika changamoto ya mikwaju ya penalti kipa wa Mtibwa, Said Mohammed 'Nduda' aliibuka shujaa baada ya kucheza penalti mbili zilizosaidia kuipeleka timu yake nusu fainali.

Nduda alizicheza penalti ya Jumaa Kassim na Abdallah Mohamed wakati zilizozama kimyani zilikuwa za Salim Abdul na Abdullah Khalisan.

Wafungaji wa matuta ya Mtibwa walikuwa ni Omar Sultan, Abdulhalim Humuod, Riffat Khamis na Dickson Job.

Kwa matokeo hayo Mtibwa Sugar nusu fainali sasa itakutana na mshindi wa mechi kati ya Jamhuri na Yanga keshokutwa kwenye Uwanja wa Amaan.

Habari Kubwa