Azam, Mtibwa zasonga mbele

08Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Azam, Mtibwa zasonga mbele

MABINGWA watetezi wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Azam FC na Mtibwa Sugar zimefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayoendelea visiwani hapa.

Azam imesonga mbele baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege katika mchezo uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan, shukrani kwa Mzambia Obrey Chirwa aliyefunga goli hilo dakika ya 56.

Akizungumzia baada ya mechi hiyo kumalizika, Kocha Msaidizi wa Azam, Iddi Cheche, alisema licha ya kupata ushindi huo, mchezo huo ulikuwa mgumu kutokana na mtindo unaochezwa katika mashindano ya mwaka huu.

Cheche alisema mtindo wa mtoano huzifanya timu kucheza kwa kutumia nguvu kubwa, ili kuhakikisha haipotezi mchezo na kusonga mbele katika kinyang'anyiro hicho.

Aidha, alisema wachezaji walijituma ili kuhakikisha wanafikia lile lengo la kusonga mbele katika michuano hii na hata kutetea ubingwa wake.

Naye Kocha Mkuu wa Mlandege, Sheha Khamis, alisema timu yake ilicheza vizuri na ilitengeneza nafasi nyingi na nzuri kuliko wapinzani wake, lakini tatizo lilikuwa katika umaliziaji.

Khamis alisema wachezaji walijitahidi katika kushambulia lakini hawakuwa bahati, huku Azam wakiitumia vema nafasi waliyoipata na kufunga bao lililowapa ushindi katika mchezo huo.

Mtibwa Sugar yenyewe ilisonga mbele baada ya kuifunga Chipukizi penalti 4-2 baada ya dakika 90 za kawaida kukamilika wakiwa sare ya bao 1-1.

Habari Kubwa