Simba, Azam FC kurudia fainali Mapinduzi ya 2019

08Jan 2020
Isaac Kijoti
ZANZIBAR
Nipashe
Simba, Azam FC kurudia fainali Mapinduzi ya 2019
  • ***Ni baada ya Bocco, Shiboub na Ajibu kuifanyia kitu mbaya Zimamoto katika Uwanja wa Gombani kwa...

MARUDIO ya mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi itashuhudiwa tena Ijumaa wiki hii katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja wakati Simba itakapokutana na Azam FC katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Mwaka jana katika michuano hiyo, timu hizo zilikutana fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba na Azam kulibeba kombe hilo baada ya kushinda kwa mabao 2-1.

Simba ambayo imefanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kuichapa Zimamoto mabao 3-1 kwenye mechi iliyopigwa Uwanja Gombani, Pemba jana, itakutana na Azam iliyoitoa Mlandege kwa bao 1-0 juzi usiku.

Katika mechi ya jana, Zimamoto ilikuwa ya kwanza kufika langoni mwa Simba na jaribio lao la kwanza lilikuwa dakika ya nne kupitia kwa Ibrahim Hilika ambaye shuti lake lilichezwa na kipa Ally Salim.

Simba ambayo ilianza kwa mchezo wa taratibu huku ikionekana kunufaika zaidi na ukubwa wa Uwanja wa Gombani kwa kucheza kwa kufunguka, ilifika langoni mwa Zimamoto kwa mara ya kwanza dakika ya tano na kuandika bao lake la kwanza.

Ilikuwa ni 'gonga' nzuri iliyoanzia kwa Hassan Dilunga na kumpasia Ibrahim Ajibu ambaye alimmegea nahodha John Bocco aliyeuzamisha mpira kimyani.

Dakika tatu baadaye kona iliyochongwa na Ajibu iliunganishwa kwa kichwa na Kennedy Juma na kuchezwa na kipa Mwinyi Hassan 'Casilas' kabla ya kumkuta Sharaf Shiboub aliyeuzamisha nyavuni.

Hassan Haji aliachia shuti kali langoni mwa Simba katika dakika ya 22, lakini Salim alikuwa makini kudaka.

Uzembe wa Erasto Nyoni wa kushindwa kufanya uamuzi wa haraka ya kucheza mpira mrefu uliopigwa langoni mwao huku akimtegea Salim adake, ulileta madhara kufuatia Hilika kumzidi ujanja na kuuzamisha kimyani dakika ya 29.

Simba ingeweza kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1, lakini mwamuzi, Seif Kesi alilikataa bao la Ajibu huku wengi wakiamini angeweza kutoa penalti kufuatia Miraji Athumani kusukumwa ndani ya eneo la 18, lakini aliamuru faulo ipigwe kuelekea langoni mwa Wekundu wa Msimbazi hao.

Akionyesha ubora wake jana, kipindi cha pili Ajibu alimchambua vema beki wa Zimamoto na kuiandikia Simba bao la tatu kwa guu lake la kulia katika dakika ya 54 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shiboub.

Simba ilifanya mabadiliko matatu dhidi ya manne ya Zimamoto kwa kumtoa Miraji Athumani na kumuingiza Rashid Juma dakika ya 68 huku dakika 10 baadaye Dilunga akimpisha nyota mpya, Luis Miquissone aliyesajiliwa dirisha hili dogo akitokea UD Songo ya Msumbiji na Ajibu akitoka dakika ya 90 kumpisha kinda Cyprian Kipenye.

Kwa matokeo hayo Simba sasa itakutana na Azam FC katika hatua ya nusu fainali itakayopigwa Ijumaa wakati Mtibwa Sugar iliyoitoa Chipukizi kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1, ikikutana na mshindi wa mchezo wa jana usiku kati ya Yanga na Jamhuri katika Uwanja wa Amaan kesho.

Simba iliwaanzisha Ally Salim, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Erasto Nyoni, Said Ndemla, Miraji Athumani/ Rashid Juma (dk.68), Sharaf Shiboub, Ibrahim Ajibu, John Bocco na Hassan Dilunga/ Luis Miquissone (dk. 78).

Habari Kubwa