Mkwasa, Kahata wang'ara Desemba

08Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mkwasa, Kahata wang'ara Desemba

KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Francis Kahata, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Desemba wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2019/2020, imefahamika.

Kahata amepata tuzo hiyo baada ya kuwazidi pointi wachezaji wenzake wawili, kiungo wa Simba, Hassan Dilunga na beki tegemeo wa Coastal Union ya jijini Tanga na Timu ya Taifa (Taifa Stars), Bakari Mwanyeto.

Kiungo huyo aliyetua Simba akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu Kenya, Gor Mahia, ameisaidia timu yake kuendeleza kasi ya ushindi na kujiimarisha katika msimamo wa Ligi Kuu ambayo huyo mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, amechaguliwa kuwa Kocha Bora wa Desemba wa Ligi Kuu baada ya kuwashinda Juma Mgunda wa Coastal Union na Sven Vandenbroeck wa Simba.

Mkwasa amekuwa na matokeo mazuri, tangu alipochukua mikoba ya Mkongomani Mwinyi Zahera, ikiwamo kuwa timu ya kwanza kuwafunga 'Maafande' wa Tanzania Prisons ambao walikuwa hawajapoteza mchezo hata mmoja msimu huu.

Kahata na Mkwasa, wataungana na washindi wengine kuwania tuzo ya mwaka itakayotolewa baada ya kumalizika kwa msimu huu wa 2019/20.

Habari Kubwa