Uamuzi wa serikali kuzibana taasisi za fedha wa kupongezwa

08Jan 2020
Mhariri
Nipashe
Uamuzi wa serikali kuzibana taasisi za fedha wa kupongezwa

MOJA ya vilio ambavyo vimekuwa vikiwagusa wananchi ni riba kubwa ya mikopo wanazotozwa kutoka katika taasisi za fedha pindi wanapopata huduma hizo.

Kilio hiki ni cha muda mrefu na miongoni mwa taasisi ambazo zimekuwa zikishutumiwa ni benki na zile ndogo zinazotoa huduma za kifedha ikiwamo mikopo kwa wajasiriamali, wafanyakazi na wananchi wa kawaida.

Sambamba na kulalamikiwa kwa taasisi hizo kuwa zinawaumiza wakopaji, pia serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ndiyo mdhibiti zimekuwa hazikwepi lawama hizo.

Hatimaye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amevunja ukimya kuhusu suala hilo huku akiweka bayana kwamba riba kubwa inayotozwa na taasisi za fedha zimekuwa zikiwaumiza wananchi.

Dk. Mpango hakuishia hapo bali amewataka watumishi wa umma ambao wanaendesha huduma ndogo za fedha na kushiriki kuwapa mzigo mzito wananchi wa madeni kutokana na mikopo kuacha mara moja vinginevyo watachukuliwa hatua pindi watakapobainika kufanya hivyo.

Hata hivyo, Dk. Mpango katika mkutano wake jana na vyombo vya habari jijini Dodoma, alielekeza nguvu zaidi kuzionya taasisi zinazoendesha huduma ndogo za fedha kuwa ndizo zimekuwa zikinyooshewa kidole na kulalamikiwa kuwa zinatoza riba kubwa za mikopo.

Waziri katika kuweka sawa juu ya hilo, alisema wazi kwamba baadhi ya watoa huduma hao wamekuwa na tabia ya kujipangia riba wanavyotaka ili kujipatia faida kwa haraka bila kujali wananchi wanaowakopesha.

Kutokana na hali hiyo, alisema huduma hizo zimekuwa kikwazo kwa wananchi wengi kwa kuwa riba zinazotozwa na baadhi ya taasisi hizi hazina tofauti na viwango vya mikopo itolewayo. Kwa maneno mengine, mwananchi anaweza kutozwa riba ya asilimia 30 na anapochelewa kulipa anakumbana na adhabu ya kutozwa asilimia fulani kwa kila siku anayochelewa kupeleka rejesho.

Pamoja na kwamba tamko la Waziri limechelewa, kitendo hicho ni cha kupongezwa kwa sababu kitawasaidia wananchi ambao wameumizwa kwa kiasi kikubwa na hata kuwa maskini kutokana na huduma hizo.

Tunasema hivyo kwa sababu baadhi ya watu wamekuwa wakikopa fedha kidogo, lakini wanaweka dhamana kubwa kulinganisha na kiasi cha mikopo wanayochukua. Matokeo yake, wanaposhindwa wanafilisiwa dhamana zao na hatimaye kupoteza mali na kurudi kwenye umaskini.

Kwa mfano, baadhi ya taasisi za fedha zimekuwa zikitoa mikopo mifupi ya mwezi ambayo huenda haizidi Sh. milioni moja kwa mkopaji lakini anatakiwa kuweka dhamana ya kadi ya gari. Magari ambayo yanatakiwa kuwa dhamana ni yake yenye namba za usajili ‘C’ na ‘D’ tu na mkopaji anaposhindwa kurejesha mkopo, ananyang’anywa gari.

Hakika uamuzi ambao umechukuliwa na serikali wa kuzionya taasisi hizo ambazo zinawanyonya wananchi kupitia kivuli cha mikopo, unapaswa kufanyiwa kazi na kuleta matokeo chanya.

Habari Kubwa