Yamepita ya elimu 2019, sekta ipige hatua 2020

08Jan 2020
Beatrice Moses
Nipashe
Yamepita ya elimu 2019, sekta ipige hatua 2020

TUMEINGIA mwaka mpya 2020, shule zimefunguliwa wiki hii. Wanafunzi wengi wakiwamo wa bweni, wameanza kurejea masomoni.

Kuna matukio kadhaa yameacha kumbukumbu katika sekta hii, yaliyoibuka mwaka 2019. Yapo yaliyokuwa mema na mengine mabaya, tena sana, kama ilivyo kwa mazuri sana.

Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kila jambo. Pia, yapo mambo ambayo ni ya ovyo, ambayo hatupaswi kwenda nayo.

Hapo nataja vitendo vya ukiukwaji maadili, ambavyo vimekuwa yakifanywa na baadhi ya wanafunzi, hivyo kusababisha kero kwa walimu, wanafunzi wenzao, wazazi na taifa kwa ujumla.

Ni wazi kila mzazi au mlezi mwenye busara na hofu ya Mungu, anapenda kusikia habari zilizo njema kuhusu  mwanawe, wapo walionunua hadi zawadi na kuwakabidhi watoto wao kwa furaha, kutokana na kutajwa katika orodha ya waliofanya mambo mazuri, ikiwamo kilichowapweleka masomoni, kufaulu kwa kiwango cha juu.

Pia kuna wazazi ambao waliojikuta katika wakati mgumu kutokana na vitendo vibaya ambayo watoto wao walitajwa kushiriki. Kuna waliolazimika kulipa fidia kwa hasara, kutokana na hatua ya kufukuzwa shule wakihusishwa na ovu shuleni.

Katika matukio yaliyoshtua na kusikitisha kwenye sekta ya elimu mwaka jana, ni linalodaiwa kufanywa na wanafunzi kadhaa wa Shule ya Sekondari Kiwanja, wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya, waliodaiwa kuchoma moto mabweni mawili shuleni hapo. Oktoba Mosi mwaka jana na kusababisha yateketee.

Sababu iliyotajwa kusababisha wanafunzi hao kuchoma moto mabwenini kutaka kulipiza kisasi, mara baada ya kunyang’anywa simu na uongozi wa shule hiyo.

Hatua kadhaa zilichukulia dhidi ya wanafunzi waliotajwa kuhusika, huku Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila, akiliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha wazazi wa watoto hao waliokutwa na simu kila mmoja analipa Sh. milioni moja zitakazotumika kukarabati mabweni yaliyoteketezwa.

Pamoja na maagizo hayo, Chalamila alifika shuleni mara moja na kuwacharaza bakora wanafunzi hao, iliyoendana na hatua zingine za kiuzazi. Picha za tukio hilo zilirushwa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mijadala mingi.  

Mkuu wa Shule, Elly Mnyarape, alibainisha kuwa chanzo cha tukio hilo ni Septemba 30, 2019 na walipofanya msako na kukamata simu 26, ndipo usiku wake mabweni yaliteketezwa kwa moto.

Ni wazi, miliki ya simu kwa wanafunzi inazuiliwa kwa nia njema, kuepusha matumizi yasiyofaa, ikiwamo kuangalia picha na video za ngono zinazowachochea kushiriki au kupotoka kitabia.

Uhuru usio na mipaka ni matatizo, hasa kwa wanafunzi wa shule za sekondari ambao bado wanahitaji uangalizi wa wazazi au walezi, ili kuwasaidia katika kuwapa mwongozo.

Wanafunzi wote wanapaswa kuheshimu sheria na taratibu za shule, ili kuepuka mambo mabaya ikiwamo kukamatwa na kuadhidibiwa ikiwamo kufukuzwa shule hatua ambayo itaweka doa na kumbukumbu mbaya itakayokuwa inawaumiza katika maisha yao.

Wazazi na walezi tuna wajibu wa kuhakikisha tunazungumza na watoto wetu ili wajue maadili mema na wazingatie mafundisho ya dini ambayo yatasaidia kuwapa mwongozo mwema hivyo kuepuka kushiriki kwenye vitendo viovu ambavyo vitawagharimu.

Pia walimu na viongozi wengine, hapo nikijumuisha Kamati za Shule, zina wajibika kuhakikisha wanasimamia vyema maendeleo ya wanafunzi na kuwapa mwongozo, utakaofanya shule zao ziwe na matokeo mazuri yakayowapa faraja na furaha, kuonyesha jinsi kazi yao ilivyo njema kwa jamii na taifa kwa ujumla.  

Aidha, upande mwingine mwaka 2019 uliandikwa historia mpya katika sekta hii ya elimu, baada ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kufanikiwa kuanzisha tuzo za elimu.

Wanafunzi bora, walimu bora, halmashauri na mikoa iliyofanya vyema kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha tano na darasa la saba walipewa tuzo.  

Hatua hiyo inatajwa itachochea kiwango cha elimu nchini, kwa kuwa itawezesha kuongezeka ushindani katika kujifunza, kufundisha, kusimamia na utekelezaji wa sera za sekta hiyo kwa ujumla.

Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya tuzo hizo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, alikabidhi tuzo kwa washindi wa nafasi mbalimbali.

Katika mwaka huu 2020, tunatamani kuona ushindani katika tuzo hizi unaongezeka ili malengo ya kuanzishwa kwake yaweze kutimia. Ni furaha kuona sekta ya elimu ikipiga hatua kwa viwango vingine vizuri.

Habari Kubwa