NEC iwape wananchi elimu endelevu kuongeza uelewa

09Jan 2020
Mhariri
Nipashe
NEC iwape wananchi elimu endelevu kuongeza uelewa

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema moja ya changamoto zonazoikabili mara kwa mara ni jamii kushindwa kufahamu au kutofautisha kati ya uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa.

Hayo yalielezwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mbarouk M’barouk, wakati akifungua mkutano wa NEC na wadau wa uchaguzi mkoani Lindi.

Jaji Mbarouk alisema yapo maeneo wananchi wake wamekuwa na mtizamo tofauti, wakifikiri uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi zote zinasimamiwa na tume hiyo, jambo ambalo sio la kweli.

Alisema uchaguzi wa serikali za mitaa unasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wakati NEC inawajibika na usimamizi wa uchaguzi mkuu pekee, ambao unahusisha rais, wabunge na madiwani.

Alisema kwa kutotambua umuhimu wa jambo hilo, Tume imeamua kushirikisha wadau kushiriki katika michakato ya uchaguzi kwa lengo la kuwa karibu nao, ili kujenga imani kwa wananchi na kuweka uwazi wa utekelezaji wa majukumu yake.

Tume bila shaka imeone kuliweka wazi suala hili kwa kuwa ni kweli kwamba wananchi wengi wanashindwa kuelewa majukumu ya chombo hicho yanaishia wapi.

Kimsingi, wengi wanaendelea kuamini kuwa majukumu ya NEC ni kusimamia na kuratibu uchaguzi wote nchini; kwa maana uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa.

Pengine ndiyo maana makundi kadhaa katika jamii yamekuwa yakipendekeza kwamba uchaguzi wa ngazi zote wa kisiasa usimamiwe na NEC, kwa hoja kuwa ndicho chombo rasmi kinachowajibika kushughulikia masuala ya uchaguzi nchini.

Kutokuwapo kwa uelewa wa jamii wa majukumu ya NEC ni jambo linaloleta tafsiri kwamba utoaji wa elimu kwa umma kuhusiana na mchakato wa uchaguzi kwa ujumla, haujawa wa kutosha.

Kutokana na hali hiyo, changamoto inayoonekana ni kwa tume yenyewe kuchukua hatua za makusudi kwa kujikita zaidi katika utoaji wa elimu ya mpigakura kwa umma kuwa endelevu badala ya kusubiri uchaguzi unapokaribia.

Katika kuonyesha ukubwa wa tatizo la jamii yetu kuelewa kuhusu taasisi za kusimamia uchaguzi, mwaka jana wakati wa kuandikisha wapigakura kwenye daftari la wakazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, kulikuwapo na mkanganyiko mkubwa.

Katika maeneo mengi wananchi walikuwa wakiamini kuwa kitambulisho cha mpigakura kinachotolewa na NEC ndicho kingetumika kupigia kura.

Mkanganyiko huo uliondoka baada ya Tamisemi kutoa matamko ya kusisitiza kuwa ndiyo inayosimamia uchaguzi huo na kuweka wazi kuwa kitambulisho cha mpigakura hakitatumika, badala yake vitatumika vitambulisho vya aina saba.

Kwa kuwa NEC imeliona tatizo hili, tunaamini kuwa itachukua hatua haraka kulitafutia ufumbuzi, kupitia utoaji wa elimu endelevu, hivyo wapigakura kutambua majukumu ya NEC na ukomo wake.

Aidha, tunaishauri Tamisemi kutoa elimu kwa umma kuhusiana na jukumu na mamlaka yake ya kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuwaondolea wananchi mkanganyiko, na kuwawezesha kushiriki kwa wingi katika uchaguzi ujao.

Tunaamini kuwa elimu endelevu ndiyo inayoweza kuwapa uelewa wananchi katika masuala yote yanayohusu uchaguzi.

Habari Kubwa