Faini za kwenye taa maumivu makubwa

09Jan 2020
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Faini za kwenye taa maumivu makubwa

JUZI katika safu hii, nilikuwa na hoja kuhusu hali inayojenga msuguano usio na msingi kati ya askari wa usalama barabarani na waendeshaji vyombo vya moto barabarani, jijini Dar es Salama. Leo pia, naendeleza hija yangu ndani ya jiji hilo.

Sehemu kuu ya hoja yangu ni namna fani zinazotozwa katika maeneo ya michoro ya wapitao kwa miguu, Zebra. Kwa kweli ujumbe mkuu ni kwamba, siridhiki nazo.

Niseme, katika makutano mengi ya barabara nyingi za Jiji la Dar es Salaam na mikoani, kuna taa za kuongoza magari, zinazowasaidia kuongoza magari kutembea kwa utaratibu maalum unaoiondoa mvurugano.

Taa hizo ni muhimu sana na inapotokea haziwaki kwa sababu mbalimbali na hakuna askari wa usalama barabarani, madereva hujikuta katika wakati mgumu sana, wakivuka mahali hapo kwa mtindo mwenye nguvu ndiye hupata nafasi.

Taa hizo na matumizi yake kisheria. Nyekundu inazuia magari kutembea, njano maana yake kaa tayari ama kuondoka au kusimama na rangi ya kijani, inaruhusu magari kutembea.

Kwenye baadhi ya mikoa kama Morogoro, taa zake zinaonyesha dakika, kwa hiyo dereva anaangalia dakika kabla ya kufanya uamuzi wa kupita au la, lakini kwenye maeneo mengine dereva, anapaswa kuangalia inapobadilika.

Kwa Jiji la Dar es Salaam, taa hizo ni maumivu kwa madereva wengi kwa kuwa nyakati zote utakuta askari wamejificha hatua chache baada ya taa na wanavizia kila gari la mwisho, kupita kwenye taa hizo kwa ajili ya kutoza faini.

Kinachofanyika, ni kumvizia dereva ahukumiwe bila kusikilizwa, kwa kuwa moja kwa moja macho ya askari ndiyo yameona kosa na ndiyo yenye jukumu la kuamua dhidi ya dereva.

Mara nyingi unapokamatwa na trafiki cha kwanza atakwambia umepita kwenye taa nyekundu na unapaswa kumkabidhi leseni ili akutoze faini, na anayekwambia kosa na kutoa hukumu ya kukutoza faini ni askari mwenyewe.

Makosa mengine kama ya kuzidisha mwendo huwa na ushahidi wa picha na kupunguza malalamiko kwa madereva, kwamba wanabambikwa makosa, lakini haya ya taa, hayana ushahidi wowote zaidi ya askari kuvizia gari ya mwisho na kuikamata.

Kwa sasa, askari wako kila mahali penye taa na wanavizia magari hasa kwenye maeneo yenye kona,

Mathalani kwenye taa za makutano ya maktaba, vivyo hivyo katika Barabara ya Morogoro, makutano ya Chuo cha DIT, katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Eneo jingine ambalo wameweka kibanda kabisa ni Salenda kuelekea Muhimbili, Oysterbay na barabara inayokatiza kuelekea Msasani, kote huko askari huwa katika mavizio kukamata gari ya mwisho.

Jambo hilo linatuogopesha sana madereva wengi kiasi kwamba unapofika kwenye taa, una gari dogo na la mbele yako ni gari kubwa, inakubidi usubiri liende umbali fulani ili uweze kuona taa ndipo upite.

Wakati mwingine unaondoka ulikokuwa umesubiri taa ikiwa kijani na ukiwa katikati au unamalizia unaona inawaka ya njano na hapo moja kwa moja askari huhesabu umekataa.

Pia, unapojaribu kujitetea, basi utaambiwa unamgomea askari na kinachofuata ni kupelekwa kituo cha polisi.

Madereva wengi kwa kuepuka usumbufu, wameandikiwa faini ambazo ni maumivu makubwa hasa kwa hali ya maisha ya leo, badala ya kuweka mafuta kwenye gari yako, unajikuta unalipa makosa ambayo ni ya kubambikiwa.

Ni vyema Jeshi la Polisi likafanya uchunguzi wa jambo hili kwamba faini za kwenye taa wanazotozwa madereva ni za haki au ni uonevu, japo nakiri wapo madereva kadhaa wasioheshimu taa hizo, hivyo kulazimishwa kutii sheria kupitia adhabu.

Nishauri, kwamba ni vyema Polisi wa Kitengo cha Usalama Barabarani, wakajadiliana na wanaoweka taa hizo na kuja na utaratibu kama unaotumika katika mikoa mingine, kwamba taa zihesabu dakika na dereva anapofika eneo hilo anaona kabisa ni dakika ngapi zimebakia kuliko, iliyopo sasa ya kubuni.

Naamini kabisa uwepo wa taa zenye kuhesabu dakika, utasaidia kupunguza malalamiko ya madereva na kuwasaidia askari kuondokana na lawama au watu kuwa na kinyongo kuwa faini wanazotozwa ni za uonevu.

Hakuna ubishi kwamba, pasipo utii wa sheria bila shuruti, hakuna barabara wala usafiri salama. Kila mtumiaji wa barabara, anapaswa kuheshimu sheria na kanuni za barabarani, kuliko kufanya anavyotaka.

Wasimamizi wa sheria hizo, nao wanapaswa kuhakikisha wanatenda haki inayoonekana imetendeka, kuliko kuonea au kutoa adhabu zisizostahili kwa madereva na ikifikia hatua ya kuwepo taa zenye kuhesabu dakika, kutasaidia sana.

Habari Kubwa