Mgunda afunguka siri ya ushindi mfululizo Coastal

10Jan 2020
Somoe Ng'itu
Nipashe
Mgunda afunguka siri ya ushindi mfululizo Coastal

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda, amesema kuwa ushirikiano na 'sapoti' wanayopata kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo ya jijini Tanga, ni moja ya sababu ya kikosi chake kufanya vizuri kwenye mechi za nyumbani za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Coastal Union ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, bao pekee katika mchezo huo likipachikwa kimyani na mshambuliaji, Ayoub Lyanga dakika ya 76.

Matokeo hayo yameifanya mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1988 wafikishe pointi 29 na kupaa hadi katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kushuka dimbani mara 16.

Mgunda, alisema kuwa juhudi za wachezaji kupambana na kutowadharau wapinzani wao, kumewasaidia kupata ushindi katika mechi nyingine na nyingine tano zilizopita.

"Kubwa zaidi ni kuwashukuru wapenzi na wanachama wa Coastal Union wa Mkoa wa Tanga kwa jinsi wanavyowasapoti vijana wangu, wamekuwa chachu kubwa ya sisi kupata matokeo," alisema Mgunda.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, alisema timu yake haikutumia vema nafasi walizotengeneza katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa wao kupata kichapo.

Maxime alisema bado hawajakata tamaa, wataendelea kurekebisha makosa yao katika mechi zinazofuata za ligi hiyo.

"Kipindi cha kwanza ndio tulipata nafasi nyingi, tukazichezea, lakini wenzetu wakapata nafasi, tena sio nafasi, tukazembea, ila keshokutwa tuna mchezo mwingine, tutapambana kusaka ushindi," Maxime alisema.

Coastal Union imeshinda mechi sita mfululizo na ilianza kutoa kichapo kwa Namungo, Ndanda, Mbeya City, Tanzania Prisons, Azam FC na Kagera Sugar hapo juzi.

Habari Kubwa