Kaseja kurejea dimbani Februari

10Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kaseja kurejea dimbani Februari

GOLIKIPA wa KMC inayoshiriki Ligi Kuu Bara na Timu ya Taifa (Taifa Stars), Juma Kaseja, amesema anatarajia kurejea tena uwanjani mapema mwezi ujao.

Kaseja alifanyiwa operesheni ya goti la mguu wa kulia hivi karibuni, baada ya kubainika kuwa na uvimbe, siku chache kabla ya kuanza kwa mashindano ya Kombe la Chalenji Desemba mwaka jana.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Kaseja alisema anaendelea vema na tayari ameanza mazoezi 'maalumu' chini ya madaktari wa Taifa Stars.

Kaseja alisema anamshukuru Mungu, amewahi kupata matibabu kabla ya tatizo lake kuwa kubwa na hivyo anatarajia kurejea uwanjani katika mechi za Ligi Kuu Bara hivi karibuni.

“Namshukuru Mungu niko vizuri, sina maumivu, na nimeshaanza mazoezi maalumu, kurudi uwanjani kamili hadi Februari," alisema kipa huyo wa zamani wa Simba, Yanga na Moro United.

Kaseja aliisaidia Taifa Stars kukata tiketi kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zitakazofanyika Aprili mwaka huu.

Habari Kubwa