BoT yawabana wakopeshaji binafsi, Vicoba

10Jan 2020
Salome Kitomari
Nipashe
BoT yawabana wakopeshaji binafsi, Vicoba

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imevitaka vikundi, kampuni au mtu binafsi wanaopokea amana au kutoa mikopo, kujisajili kabla ya Oktoba 31, mwaka huu.

Aidha, imesema mtu yeyote atakayekutwa anatoa huduma hizo bila leseni atachukuliwa hatua za kisheria, huku ikibainisha kuwa usajili ulianza Novemba Mosi, mwaka jana.

"BoT inatoa onyo kwa mtu, kikundi au taasisi yoyote inayojihusisha na biashara ya upokeaji amana na/au utoaji wa mikopo bila kuwa na leseni kuacha mara moja," ilisema taarifa hiyo jana.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, kinakataza mtu yeyote kufanya biashara ya kibenki au kupokea amana kutoka kwa umma bila kuwa na leseni kutoka BoT.

Ilifafanua kuwa kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya 2018, kinakataza mtu binafsi, kampuni au kikundi kilichoanza biashara kuanzia Novemba Mosi, mwaka jana kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila kuwa na leseni halali inayotolewa na benki hiyo.

"Wananchi wanaombwa kutoa taarifa BoT, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pale wanapopata taarifa za uwepo wa watu binafsi, makampuni au vikundi vinavyotoa huduma za fedha bila kuwa na leseni," ilisisitiza.

MMILIKI VICOBA MBARONI

Katika hatua nyingine, BoT imebainisha uwapo wa kampuni za kitapeli zinazodai kutoa mikopo kwa wananchi ndani ya muda mfupi baada ya kujiunga kwa kuweka amana kwa njia ya mtandao.

Tarifa hiyo ilibainisha kuwa kampuni mojawapo ni Vicoba Foundation ambayo inajinasibu kuwa kutoa mikopo ya kuanzia Sh. milioni mbili hadi 10 baada ya mteja kulipia ada ya kujiunga ya kati ya Sh. 200,000 hadi 500,000.

"Ili kuvutia wananchi kampuni hii imekuwa ikiudanganya umma kwamba ni taasisi ya serikali, jambo ambalo halina ukweli wowote. Uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba kampuni hii haina ofisi ya kudumu," ilibainisha na kuongeza:

“Kampuni hiyo inadaiwa kutumia majina ya viongozi wakuu wa nchi na watu mashuhuri katika kufanikisha utapeli wao.”

Majina waliyodaiwa kuyatumia ni Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hasan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

"BOT inapenda kuufahamisha umma kwamba mmiliki wa Vicoba Foundation kwa sasa anashikiliwa na vyombo vya dola ambavyo vinaendelea na uchunguzi ili kuchukua hatua stahiki," ilifafanua.

Habari Kubwa