DC asimulia askari alivyojitoa muhanga kufunga valvu mafuta

10Jan 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
DC asimulia askari alivyojitoa muhanga kufunga valvu mafuta

MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, amesimulia askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji alivyojitosa katikati ya moto kwenye matangi ya kuhifadhia mafuta ya kampuni ya Lake Oil na kufanikiwa kufunga valvu iliyokuwa inavuja mafuta na kuudhibiti.

Akizungumza JANA katika eneo la tukio, Kigamboni, Jijini Dar es Salaam, Msafiri alisema  baada ya kufika eneo hilo na kushuhudia moto ukiwa unasambaa kwa kasi, askari huyo aliamua kuingia katikati ya moto na kwenda kufunga valvu  katika moja ya matangi hayo baada ya kuona inatoa mafuta.

"Askari wetu alishuka chini kwa kujitolea na moshi na moto chini, akashuka akajitosa kuingia katikati ya moto ili kuokoa maisha ya maelfu ya wakazi wa Kigamboni. Kwa hiyo hali imetulia kwa sababu ya askari huyu mzalendo,"alisema Msafiri.

"Lakini si kuokoa wana-Kigamboni na Watanzania tu, bali hata kuokoa uchumi wa nchi zaidi ya sita ambazo zinapata mafuta kupitia Tanzania.

"Mafuta, gesi, 'depot' yao kubwa ni hapa Kigamboni Vijibweni. Tuna 'supply' (sambaza) mafuta ndani ya nchi na zingine sita zinazotuzunguka. Kwa hiyo unaweza kuona uzalendo ambao askari wetu anao."

"Ameonyesha kwamba pale inapotokea kwamba ipo haja ya kuokoa taifa, inabidi ujitoe muhanga. Tumefanikiwa kudhibiti moto, askari wetu 'ame-faint' lakini anaendelea vizuri. Nimshukuru Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji  wamejipanga vizuri na kuna timu imebaki kwa ajili ya kusoma  mazingira,” alisema Msafiri.

Alisema walibaini kwamba moja ya valvu ilikuwa inavuja katika matangi hayo ya mafuta na kwamba bado wanafanya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

"Kilichokuwa kinachochea moto kukua ilikuwa valvu kuvuja, lakini chanzo chenyewe cha moto kutokea bado hakijafahamika. Bado uchunguzi unaendelea na utakapokamilika tutafahamishana kitaalamu,"alisema.

Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Temeke, Elia Kakwembe, alisema licha ya kuzima moto huo, bado timu maalum iliachwa jana katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya uchunguzi ili kufahamu chanzo cha moto huo.

"Tunaendelea kufanya uchunguzi na tutafanya wa kina kubaini nini chanzo cha moto. Hiyo itatusaidia kupunguza majanga mengine ya namna hii, tunachoshukuru hakuna majeraha makubwa,"alisema Kakwembe.

Habari Kubwa