JPM kuanza ziara Zanzibar leo

10Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
JPM kuanza ziara Zanzibar leo

RAIS John Magufuli jana aliwasili jijini Dar es Salaam akitokea nyumbani kwake Chato mkoani Geita na leo anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi visiwani Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kuwa Rais Magufuli leo ataanza ziara ya kikazi visiwani huko, akitarajiwa kuweka jiwe la msingi la jengo la Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar.

Ilielezwa katika taarifa hiyo ya Ikulu kuwa, kesho Rais Magufuli ataweka jiwe la msingi la Shule ya Sekondari ya Mwanakwerekwe iliyoko Mjini Magharibi na atafungua hoteli yenye hadhi ya nyota tano iitwayo Hotel Verde Azam Luxury Resort and Spa iliyoko Mtoni.

"Mheshimiwa Rais Magufuli atashiriki sherehe za maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zitakazofanyika Jumapili Januari 12 mwaka huu katika Uwanja wa Amaan, Mjini Magharibi," ilielezwa katika taarifa hiyo ya Ikulu.

Habari Kubwa