Waziri aishukia halmashauri kupima viwanja 105 miaka 40

10Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
LINDI
Nipashe
Waziri aishukia halmashauri kupima viwanja 105 miaka 40

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ameishukia Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi, kwa kuwa na viwanja 105 ndani ya miaka 40.

Dk. Mabula alikutana na kadhia hiyo juzi akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika Halmashauri za Mkoa wa Lindi.

Alisema pamoja na halmashauri hiyo kuwa ya siku nyingi, imeshindwa kupima maeneo na kuwamilikisha wananchi jambo lililosababisha hadi leo kuwa na hati 105 pekee.

Licha ya hatua hiyo kuikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi, Dk. Mabula alisema hatua hiyo pia inasababisha wananchi kutokuwa na miliki za viwanja, hivyo kuwakosesha fursa ya kujiendeleza kiuchumi kupitia hati za ardhi ambazo zingetumika kuchukulia mikopo benki.

“Halmashauri ina viwanja 105 wakati ni ya siku nyingi. Hii inaonyesha watumishi wa sekta ya ardhi hawafanyi kazi yao ipasavyo. Hapa kuna uzembe, Mkurugenzi fuatilia suala hili kwani vifaa vya upimaji vipo katika kanda, tatizo ni nini?” Alihoji.

Aidha, Naibu Waziri alishangazwa na Halmashauri  ya Mtama ambayo katika kipindi cha mwaka mmoja imeandaa hati mbili tu za ardhi jambo alilolieleza kuwa linampa shaka na utendaji wa watumishi wa sekta hiyo katika halmashauri hiyo.

Kutokana na hali hiyo, ameiagiza Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kusini kuiangalia halmashauri hiyo na kuisaidia katika masuala ya ardhi ikiwamo kupima maeneo ili kuwa na idadi kubwa ya viwanja vilivyopimwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Methew Makwinya na Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali, walimweleza Naibu Waziri Mabula kuwa eneo kubwa katika halmashauri hiyo halijapimwa na kubainisha kuwa njia pekee ya kuwasaidia wananchi wa Mtama ni kuwapatia timu ya wataalamu watakaosaidia kupanga, kupima na kumilikisha maeneo na hatimaye kutoa hati zikiwamo za kimila.

Walimwomba Naibu Waziri kuangalia namna fukwe zilizomo kwenye halmashauri hiyo zitakavyowanufaisha wamiliki wake kwa kuwapatia hati zitakazowasaidia kiuchumi.

Akiwa mkoani Lindi, Dk. Mabula aitembelea pia Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na Manispaa ya Lindi. Katika Halmashauri ya Ruangwa, alikagua masijala ya ardhi na kubaini majalada ya hati takriban 300 yakiwa hajakamilishwa kwa ajili ya kutoa hati kwa wamiliki wake kwa muda mrefu.

Kutokana na hali hiyo, aliipa miezi mitatu Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Ruangwa kuhakikisha inawatafuta na kuwamilikishi waombaji wote na kupatiwa taarifa kuhusiana na suala hilo.

Kwa upande wa Manispaa ya Lindi, alisikitishwa na halmashauri hiyo kushindwa kuwafuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi na wadaiwa hao kupelekewa ilani za madai.

Kwa mujibu wa Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Lindi, Andrew Munisi, ofisi yake ilipeleka hati za madai 245 zenye thamani ya Sh. bilioni tatu na baadhi ya wadaiwa wamelipa zaidi ya Sh. bilioni mbili, huku Sh. bilioni moja zikiwa bado hazijalipwa.

Habari Kubwa