Simba, Azam ngoma nzito

10Jan 2020
Isaac Kijoti
ZANZIBAR
Nipashe
Simba, Azam ngoma nzito
  • ***Makocha waahidi mawili mawili, mmoja soka la akili na kimwili, mwingine ufundi na utaalamu, huku...

BAADA ya nusu fainali ya kwanza kati ya Yanga na Mtibwa Sugar kushuhudiwa jana usiku katika Uwanja wa Amaan, mtifuano mkali wa wanafainali wa mwaka jana wa Kombe la Mapinduzi, Simba na Azam FC utashuhudiwa leo.

Katika fainali ya michuano hiyo iliyopigwa mwaka jana kwenye Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kufanikiwa kutetea ubingwa huo.

Hivyo, Simba ambayo katika mchezo huo haikuwa na nyota wake wa kikosi cha kwanza, katika mechi ya leo itakayopigwa Uwanja wa Amaan saa 2:15 usiku, itahitaji kulipa kisasi huku Azam ikipania kuendeleza ubabe na kutetea ubingwa wao.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Amaan visiwani hapa jana, makocha wa timu hizo kila mmoja alikiri mchezo huo utakuwa mgumu.

Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema itakuwa ni mechi ngumu kwa kuwa Azam imewekeza katika mchezo huo na inacheza soka la kiushindani.

Matola alisema wamejiandaa vizuri na mashabiki watarajie soka safi la kutumia akili na kimwili zaidi tofauti na mechi ya awali dhidi ya Zimamoto

Matola alisema tayari wachezaji walioanza kikosi cha kwanza dhidi ya Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ambao walibaki jijini Dar es Salaam wamewasili tangu juzi na kuungana na wenzao.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuwapo mabadiliko katika kikosi kilichoivaa Zimamoto, Matola alisema "Ndiyo, mechi ni nyingi lazima kuwapo na mzunguko wa wachezaji ili waweze kupumzika.

"Lakini kutokana na suala la kiufundi, tunajua Azam ni timu nzuri na wanataka kutetea ubingwa wao, na sisi tunachotaka ni kutwaa kombe."

Naye Kocha wa Makipa wa Azam FC, Iddi Aboubakar, alisema wanaiheshimu Simba ni timu kubwa lakini wao wamekuja kupambana na wanatarajia mechi hiyo itakuwa ni yenye ufundi mkubwa na utaalamu wa hali ya juu kwa kila upande.

Alipoulizwa mashabiki watarajie kuona Azam ikipata tena tabu ya ushindi kama ilivyoshinda kwa mbinde dhidi ya Mlandege, Abubakar alisema utakuwa mchezo tofauti kabisa.

"Unajua mechi ya kwanza kwenye mashindano yoyote mara nyingi timu inaanza kwa kujisuasua, lakini mashindano yanavyoendelea wachezaji nao wanabadilika.

"Halafu tambua unapocheza na timu ndogo nazo zinakamia sana, lakini mchezo dhidi ya Simba utakuwa wa kiufundi na kiutaalam zaidi," alisema.

Simba imetinga nusu fainali baada ya kuitoa Zimamoto kwa mabao 3-1 katika mechi ya Kundi B, wakati Azam iliyokuwa Kundi A, iliitoa Mlandege kwa bao 1-0.

Fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kupigwa Jamatatu saa 2:15 usiku katika Uwanja wa Amaan.

Habari Kubwa