Kocha mzungu atua Jangwani

10Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kocha mzungu atua Jangwani

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Black Leopard ya Afrika Kusini Mbelgiji Luc Eymael amewasili nchini tayari kuanza kuifundisha Yanga inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, imefahamika.

Kocha huyo atatua nchini kuchukua mikoba iliyoachwa na Mkongomani Mwinyi Zahera, ambaye nafasi yake ilishikiliwa kwa muda na Boniface Mkwasa.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema baada ya kuwasili nchini, watakamilisha mazungumzo haraka ili aweze kuanza kazi ya kukinoa kikosi hicho kinachopambana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Bumbuli alisema wanaamini ujio wa mbelgiji huyo utasaidia kufikia malengo ya klabu hiyo kwa msimu huu, baada ya kuimarisha kikosi chao katika dirisha dogo la usajili.

"Ni furaha yangu kuona nimepata timu kubwa ndani ya Afrika. Ninaitambua vema falsafa yake na namna ilivyo, hivyo nina imani tutakwenda nayo sawa," alisema kwa kifupi Eymael baada ya kuwasili.

Baadhi ya timu alizowahi kufundisha kocha huyo ni AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Missile (Gabon), AFC Leopard (Kenya), Rayon Sport (Rwanda, JS Kairouan (Tunisia), El Merreikh (Sudan), Polokwane City na Free State Stars za Afrika Kusini.

Habari Kubwa