Mwanafunzi aliyeongoza afunguka mazito

10Jan 2020
Elizaberth Zaya
Nipashe
Mwanafunzi aliyeongoza afunguka mazito

MWANAFUNZI aliyeshika nafasi ya kwanza katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Francis jijini Mbeya, Joan Ritte (17), ametoa ya moyoni baada ya kutangazwa matokeo hayo.

Akizungumza na Nipashev jana , Joan alisema siri ya kupata matokeo hayo mazuri ni kujituma kwenye masomo, jitihada za walimu katika kuwafundisha, jitihada za wazazi kumsimamia na msingi wa hofu ya Mungu.

"Sikutegemea kama ningepata matokeo haya leo. Safari ya elimu tangu nijiunge na shule hii haikuwa mbaya. Siku zote nilikuwa sitoki katika 'top four' (wanne bora) lakini sikutegemea kama leo hii ningekuwa mbele kuliko wenzangu. Nilikuwa naona hizo nafasi ni za watu wengine tu," alisema Joan na kuongeza:

"Kabla ya mtihani nilikuwa nimejiandaa kiasi nikajiamini kwamba nitafaulu lakini ilipofika siku yenyewe ya mtihani, nilipatwa kidogo na hofu ya mtihani. Niliwaza kwamba huu ndio mwanzo wangu wa kuandaa maisha na je, nisipofanya vizuri itakuwaje. Lakini nilikumbuka msingi wa imani ambao tumejengewa shuleni, nilimwamini Mungu nikapata nguvu, nikafanya mtihani wangu vizuri.

"Sitaisahau katika maisha yangu yote ile shule yangu. Mwanzoni wakati naingia pale nilikuwa si mtu wa kusali sana lakini kutokana na misingi iliyoko pale nilijikuta ni mwombaji mzuri maana ilikuwa kama sehemu ya mambo muhimu pale na ilinisaidia kunijengea msingi mzuri wa maisha. Nilifundishwa nidhamu ya hali ya juu na namna ya kuishi na watu wote na kujituma kwa kila jambo. Kwa hiyo ukichanganya na msaada mkubwa niliokuwa napewa na wazazi wangu vilinisaidia sana."

USHAURI WA DADAYE

Alisema jambo lingine ambalo lilichangia kufanya kwake vizuri ni dada yake ambaye naye katika mtihani wake wa mwisho wa kidato cha nne, aliingia katika nafasi ya wanafunzi 10 bora.

"Kitu kingine ambacho kiliniongezea nguvu na kuona hata mimi ninaweza, ni dada yangu ambaye aliwahi kufanya vizuri na kushika nafasi ya 10 kwa wasichana waliokuwa wamefanya vizuri kitaifa katika mtihani wao, nilihakikisha na mimi nakazana angalau nifike hapo, kwa sababu pia wazazi wangu na ndugu walikuwa wananihusia hivyo na kunitolea mfano huo kila mara.

"Lakini ninachoshukuru dada yangu naye alivyoona hivyo alijua nitapaniki, akanituliza kwa kuniambia nisisikilize maneno ninayoambiwa na watu kwamba nisipambanie matokeo wanayotaka wao, bali nihakikishe natumia uwezo wangu na kumtegemea Mungu.

Nililishika sana lile neno na nilipoingia kwenye chumba cha mtihani nilitulia, niliomba Mungu anisaidie kuniondolea zile sauti nilizokuwa naambiwa kwamba lazima nifanye kama alivyofanya dada yangu," alisema.

SAFARI YA MAISHA

Joan alisema anatoka katika familia ya baba na mama ambao ni watumishi wa umma wenye maisha ya kawaida.

"Baba yangu ni mhasibu katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na mama ni mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi ."

MWALIMU ATOA NENO

Mwalimu wa shule hiyo, Leonard Peter, alisema siri kubwa iliyochangia wanafunzi wa shule hiyo kufanya vizuri ni mazingira mazuri ya kazi waliyojengewa wafanyakazi wake.

Nyingine ni kazi kubwa inayofanywa na walimu katika shule hiyo katika kuwafundisha wanafunzi kwa bidii, kuwajengea misingi mizuri ya hofu Mungu na nidhamu.

MAMA MZAZI ANENA

Kwa upande wake mama mzazi wa Joan, Marina Mkonyi alisema matokeo ya mtoto wao yamewapa faraja kubwa.

"Si kwamba hatukutegemea kwamba angefaulu, tulijua atafaulu vizuri kwa sababu ripoti zake zote za shuleni hakuna alipowahi kufeli, isipokuwa hatukujua kwamba angeongoza kabisa,"alisema mama mzazi wa mwanafunzi huyo.

Alisema kama wazazi siku zote walikuwa wanahakikisha anakuwa na nidhamu katika kila kitu awapo shuleni.

"Mimi ni mwalimu, kwa hiyo siku zote nilikuwa namsihi kwamba zote ni mbwembwe tu, lakini vitu muhimu vinavyosaidia mwanamke aheshimike ni kuwa na elimu nzuri, kwa hiyo alikuwa analijua hilo na alikuwa anakazana kweli," alisema.

"Mwanangu huwa anashukuru sana anapopatiwa zawadi hata kama ni ndogo, kwa hiyo nilikuwa nachochea na vitu vya namna hiyo, kipindi cha mitihani yake nilikuwa nampa ahadi ya zawadi mara moja moja, kwa hiyo ilikuwa lazima nitimize kwa sababu alikuwa anafaulu," aliongeza.

Mkonyi alisema mbali na kwamba kulikuwa na umuhimu wa kuzingatia masomo, lakini alihakikisha anamfundisha kufanya shughuli zote za nyumbani anapokuwa likizo.

"Unajua na malezi pia kwa watoto wetu huwa yanasaidia. tusipende kuwasikiliza kila kitu wanachotuambia au wanachotaka, tunawaharibu. Mimi mwanangu sikumlea kama mayai, shughuli zote za nyumbani anafanya na haya matokeo tumeyapata nikiwa nimempa kazi ngumu za kufanya hapa nyumbani.

Habari Kubwa