330 wafutiwa matokeo

10Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
330 wafutiwa matokeo

BARAZA la Mitihani (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 333 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani yake ya upimaji ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne mwaka jana.

Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk. Charles Msonde, alibainisha kuwa kati ya watahiniwa hao, 142 ni wa darasa la nne, 29 ni wa kidato cha pili na 162 ni wa kidato cha nne.

Alisema baraza hilo pia limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 538 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya upimaji au mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.

"Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya upimaji au mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka huu.

"Waliopata fursa hii ni watahiniwa 78 wa upimaji wa kitaifa wa darasa la nne, 225 ni wa upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili na 235 ni wa mtihani wa kidato cha nne.

Alisema takwimu za matokeo hayo zinaonyesha kuwa watahiniwa wamefanya vizuri zaidi katika masomo mengi ya msingi ambapo ufaulu wa masomo uko juu ya wastani kati ya asilimia 51.25 na 91.31.

"Takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa watahiniwa hawakufanya vizuri katika masomo mawili ambayo ni Fizikia na Hesabu, japokuwa katika somo la Fizikia ufaulu umeendelea kuimarika kutoka asilimia 45.5 kwa mwaka 2018 hadi asilimia 48.38 mwaka 2019," alisema.

Dk. Msonde alitumia fursa hiyo kueleza kuwa matokeo hayo hayajachelewa kutolewa na kwamba yametoka kwa mujibu wa taratibu zao za baraza na kuitaka jamii kutumia mitandao ya kijamii inavyotakiwa badala ya kufanya upotoshaji.

Habari Kubwa