Kilio, kicheko matokeo kidato cha nne

10Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kilio, kicheko matokeo kidato cha nne

BARAZA la Mitihani (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, yakionyesha sura mbili za 'kilio na kicheko' kwa wahusika.

Wakati wasichana wakiendelea kuongoza kwa ufaulu kitaifa, upande wa pili wa sarafu unaonyesha wavulana wamezidiwa tena katika nafasi 10 za watahiniwa bora kitaifa.

Katika kile kinachoonyesha hali si nzuri kwa watahiniwa wa kiume, safari hii wasichana wanane wameingia katika orodha ya watahiniwa 10 bora zaidi kitaifa.

Matokeo hayo yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk. Charles Msonde, yakionyesha kuwa kati ya wasichana wanane walioingia katika orodha ya wakali 10 kitaifa, saba wanatoka shule moja ya St. Francis Girls ya Mbeya.

Mtahiniwa Joan Ritte kutoka shule hiyo ndiye ayeibuka kidedea zaidi kitaifa kwa mwaka 2019.

Baraza pia limeanika orodha ya shule 10 zilizoongoza ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo ni Ibun Jazar Islamic (Pwani), St. Achilleus Kiwanuka Kijwire (Kagera), Mlalo (Tanga), Paramiho Girls (Ruvuma), Huruma Girls (Dodoma), St. Augustine Tagaste (Dar es Salaam), Nyaishozi ( Kagera), Waja Boys (Geita), Boniconsili Mabamba Girls (Kigoma) na St. Getrude Mlandizi Girls (Pwani).

Wakati shule hizo zikiendelea kufanya vizuri, baraza limetaja orodha nyingine ya shule 10 zilizoshuka ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo kuwa ni Mbwego (Tanga), Mbezi Beach (Dar es Salaam), Maahad Istiqama (Kusini Unguja), Mwaniko (Mwanza), Nyamtelela (Mwanza), Gombe High School (Kigoma), Alliance Rock Army (Mwanza), Ndomba (Kagera), Glorious Academy (Mjini Magharibi) na Kirinjiko Islamic Seminary (Kilimanjaro).

Mikoa pia haijaachwa nyuma, Necta ikieleza kuwa mikoa mitatu iliyofanya vizuri zaidi kwa sasa ni Kilimanjaro, Arusha na Iringa na iliyoongeza ufaulu kwa kipindi cha miaka mitatu ni Iringa, Njombe na Ruvuma.

Baraza pia limetoa orodha ya halmashauri 10 zilizoongoza ufaulu kwa miaka mitatu ambazo ni Madaba (Ruvuma), Mbinga (Ruvuma), Mafinga (Iringa), Bukoba (Kagera), Mpimbwe (Katavi), Pangani (Tanga), Kasulu (Kigoma), Iringa (Iringa), Njombe (Njombe) na Kilolo (Iringa).

Wakati viongozi wa halmashauri hizo wakifurahia taarifa hizo, sura nyingine ya huzuni iko kwa viongozi wenzao katika halmashauri 10 zilizoshuka kiufaulu kwa miaka mitatu.

Kwa mujibu wa Dk. Msonde, halmashauri hizo ni Mafia (Pwani), Kibiti (Pwani), Geita (Geita), Kakonko (Kigoma), Kondoa (Dodoma), Mpanda (Katavi), Kishapu (Shinyanga), Kiteto (Manyara), Bumbuli (Tanga) na Malinyi (Morogoro).

Habari Kubwa