Mungu ibariki Tanzania kuelekea fainali za Dunia

11Jan 2020
Mhariri
Nipashe
Mungu ibariki Tanzania kuelekea fainali za Dunia

KWA mara nyingine, bendera ya Tanzania kupitia mchezo wa soka inatarajiwa kupeperushwa katika kampeni ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa wanawake wa umri chini ya miaka 17.

Fainali hizo zitakazosimamiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), zitafanyika baadaye mwaka huu huko nchini India.

Katika safari hiyo, kikosi cha Tanzania ambacho kiko chini ya Kocha Mkuu, Bakari Shime 'Mchawi Mweusi' kitaanza kampeni hiyo kesho kwenye Uwanja wa Taifa kwa kuwakaribisha wenzao kutoka Burundi, huku wakitarajiwa kurudiana baada ya wiki moja mjini Bujumbura.

Ili malengo ya nchi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), yatimie, ni wakati wa mashabiki kutoka sehemu mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuwashangilia vijana hawa ambao wanahitaji kuanza vizuri mashindano hayo, wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani.

Kama tunavyoamini na kukubali kwamba shabiki ni mchezaji wa 12, tunatakiwa tujitokeze kwa wingi kwenda kuwashangilia mabinti hawa ambao hapo baadaye tunatarajia kuwaona kwenye kikosi cha wakubwa maarufu Twiga Stars.

Timu hii ikiwa nyumbani, tunatakiwa kuitendea haki kwa kufika uwanjani kuwashangilia na kudhihirisha wako kwenye ardhi ya nyumbani kwa kuwaunga mkono kuwashangilia katika muda wote wa mchezo.

Nipashe inawaomba wadau wa michezo yote walioko jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani kujitokeza kuwashangilia mabinti hawa ili wafanye vema kama walivyofanikiwa kupeperusha vizuri bendera ya nchi katika mashindano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika kwa kushirikisha timu sita za Afrika Mashariki na Kati kwa kumaliza kwenye nafasi ya pili.

Hakuna timu ambayo inaweza kupata mafanikio kama haitakuwa karibu na mashabiki wake, ukaribu na mashabiki huwafanya wachezaji kujiona wana deni la kusaka matokeo chanya na hali hii huwaongezea ari katika kupambana kusaka ushindi.

Tunaamini kwa upande wa ufundi, shime na benchi lake limekamilisha programu zote muhimu kuelekea mchezo huu wa kwanza, huku ikiyafanyia kazi upungufu uliyojitokeza wakati timu hizo zilipokutana Jinja, Uganda na matokeo kuwa sare ya mabao 3-3.

Kutopoteza mchezo hata mmoja kwenye mechi sita ilizocheza huko Uganda, ni dalili nzuri kwamba wachezaji wa timu hii wameiva na wanatakiwa kuingia uwanjani kesho wakiwaheshimu wapinzani wao.

Ni makosa kuingia uwanjani ukiwa na matokeo mfukoni, tunawaombea vijana wetu washuke dimbani wakifahamu Watanzania wanahitaji kupata ushindi na hatimaye kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele, huku wakifahamu watakuwa na kibarua kizito endapo wataiondoa Burundi.

TFF pia kwa upande wao inatakiwa kukamilisha majukumu yote ya kiutawala na kinachosubiriwa ni mchezo.

Uamuzi wa TFF kutoweka kiingilio katika eneo la mzunguko ambalo ndilo linaingiza idadi kubwa ya mashabiki, halijafanywa kimakosa, uamuzi huu umelenga mashabiki na haswa wanawake kufika uwanjani kuwashangilia watoto wao ambao wanapeperusha bendera ya nchi.

Hakuna mafanikio ambayo yatapatikana bila ya uwekezazi sahihi, kufanya vizuri kwa timu hii, ni ishara nzuri kwa Tanzania kutawala kwenye soka la wanawake kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Soka halihitaji miujiza, tunaamini mafunzo waliyopokea wachezaji wa timu hii na mechi za kirafiki walizocheza, yatatupatia matokeo chanya katika mechi ya kesho.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki kikosi cha vijana cha wanawake cha U-17.

Habari Kubwa