Maneno ya mwenda wazimu…

11Jan 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Maneno ya mwenda wazimu…

NAPENDA sana methali tulizoachiwa na wahenga wetu. Kila nisomapo hutafakari sana jinsi walivyojaaliwa hekima na Mwenyezi Mungu. Yote waliyosema enzi zao ndio yatokeayo sasa.

‘Shabiki’ ni mtu mwenye mapenzi na hamasa kubwa ya jambo au kitu. Mfano ni mashabiki wa kandanda duniani kote ingawa hapa nawazungumzia mashabiki wa Simba na Yanga, kabla na baada ya mechi zinazowakutanisha.

Januari 4, 2020 Simba na Yanga zilipambana kwa mara ya kwanza katika msimu wa Ligi Kuu inayoendelea sasa.

Husemwa “Maneno ya mwenda wazimu hayana maana lakini ni maneno.” Maana yake maneno asemayo kichaa hayana maana kwake lakini ni maneno.

Twakumbushwa kwamba inafaa kusikiliza maneno yasemwayo na watu wengine hata kama tunawadharau kwa kuwa huenda yakawa na busara fulani.

Kabla ya pambano la Simba na Yanga mashabiki wa pande zote mbili walikuwa na maneno mengi ya kejeli (maneno ya kuonyesha dharau) kwa timu pinzani.

Mashabiki wa Simba ndiwo waliokuwa na maneno mengi sana dhidi ya Yanga. Walikuwa na kila sababu ya kuwatambia wenzao kwa jinsi timu yao ilivyo na wachezaji mahiri.

Wachezaji wao wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na kuifanya timu yao iongoze Ligi Kuu kwa mabao mengi ya kufunga na machache ya kufungwa. Simba ina alama nyingi zaidi ya timu zote 20 zinazoshiriki Ligi Kuu, ikiwamo Yanga.

Kwa upande wa Yanga, ni mashabiki wachache wenye mioyo isiyo na wasiwasi walioweza kupambana na wenzao wa Simba kujibu mapigo. Wakati Simba wakisema Yanga ingefungwa si chini ya mabao 6-0, Yanga walijibu wakisema himaya ya Simba itashushwa, na Yanga kutwaa nafasi hiyo!

Maneno ya Simba yaliwaogofya baadhi ya mashabiki wa Yanga na kuwafanya kutokwenda uwanjani kushuhudia jinsi timu yao itakavyopigwa mabao 6-0 na Simba! Haikushangaza kuona Simba wakiwa wengi zaidi uwanjani.

Kwa wafuatiliaji wa mapambano ya Simba na Yanga, wanajua kuwa mara nyingi timu dhaifu ndio huishinda timu iliyokamilika kiuchezaji. Hutokea mara nyingi hata kuwashangaza watazamaji wa pande zote mbili.

Baada ya kile kisichotegemewa kufanyika, ndipo maneno ya “ilikuwaje …imekuwaje” husikika kwa mashabiki na wanachama wa timu hizo.

Wahenga walisema “Maneno makali hayavunji mfupa” wakiwa na maana kuwa maneno tu hayawezi kuvunja mifupa hata yakawa makali kiasi gani.

Kadhalika ilisemwa na wahenga kuwa “Maneno ni daraja, hayazuii maji kuteremka.” Maana yake daraja haliwezi kuyazuia maji ya mto yasiteremke. Kadhalika maneno nayo hayawezi kumzuia mtu kufanya jambo aliloazimia.

Kipindi cha pili kilipoanza, Simba ilifunga bao la pili lililofanya mashabiki wa Simba washangilie kwa hoihoi za kila aina huku wenzao wa Yanga wakiduwaa wasijue kinachoendelea!

Yanga ilipata bao la kwanza na la pili kwa muda usiozidi dakika saba. Sasa ikawa zamu ya mashabiki wa Yanga kutamba kwa nderemo huku wenzao wa Simba wakipigwa na bumbuazi (hali ya kutulia kimya kwa muda bila ya kujua la kufanya; butaa, mzubao).

Kwa hakika ni tukio ambalo halikutegemewa na mashabiki wa Yanga. Kabla ya kurejesha mabao hayo, wapo waliokata tamaa na kuanza kuondoka lakini bao la kusawazisha na kuwa 2-2 liliwarejesha uwanjani kwa shangwe!

Je, wanachama na mashabiki wa pande zote mbili wanasahau mwaka Yanga ilipoifunga Simba mabao 3-0 kipindi cha kwanza, lakini Simba ikasawazisha kipindi cha pili na kufanya matokeo kuwa sare ya 3-3 mpaka mwisho wa mchezo? Wakati ule kocha wa Simba alikuwa Abdallah Kibadeni.

Huu ndio ubishi na tambo nilizokuta katika moja ya mitaa ya Kariakoo majuzi. Shabiki wa Yanga alikuwa akitamba kwa timu yake kurejesha mabao mawili ya Simba kwa muda mfupi kuliko yaliyofungwa na Simba kwa kila kipindi bao moja.

Shabiki wa Simba alibeza sare ya timu hizo kwa kuwatusi (sipati herufi za kuandika neno chafu alilosema shabiki huyo)Yanga akisema: “eti Yanga kusawazisha kwao ndio ushindi …” kisha akatoa tusi zito kwa watu wa Jangwani wanaosherehekea sare!

Waingereza husema kandanda ni mchezo wa kubahatisha. Naam, timu yaweza kucheza vizuri sana kama walivyokuwa Simba, lakini ikashindwa na timu inayobezwa na watazamaji. Ndio mambo ya ushindani, hasa mchezo wa kandanda.

Mchezo wowote ni jambo ambalo watu au timu hulifanya kwa kushindana ili kujifurahisha na kuwafurahisha watazamaji hasa timu moja inapopata ushindi. Hakuna sababu ya kuchukiana, kutukanana wala kupigana!

Habari Kubwa