Kakolanya aanika 'uchawi' wa kucheza penalti ulipo

13Jan 2020
Isaac Kijoti
ZANZIBAR
Nipashe
Kakolanya aanika 'uchawi' wa kucheza penalti ulipo

KIPA aliyetokea kukubalika zaidi kwa sasa na mashabiki wa Simba, Beno Kakolanya ameweka bayana siri kubwa katika kuicheza mikwaju ya penalti.

Katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam FC iliyopigwa Uwanja wa Amaan Ijumaa iliyopita, Kakolanya aliibuka shujaa wa Simba baada ya kuipeleka fainali.

Kakolanya alicheza penalti ya mwisho ya Azam iliyopigwa na kipa mwenzake Mghana Razack Abalora na kufanya Simba kutinga fainali ya michuano hiyo kwa penalti 3-2 baada ya matokeo ya suluhu ndani ya dakika 90.

Kwa matokeo hayo, Simba sasa itakutana na Mtibwa Sugar leo katika mechi ya fainali itakayopigwa Uwanja wa Amaan leo saa 2:15 usiku.

Akizungumza na Nipashe, Kakolanya alisema uchawi wa kucheza penalti ni kufanya mazoezi zaidi na hiyo ndiyo imekuwa siri ya mafanikio yake.

Kipa huyo alisema kwenye mazoezi amekuwa akifanyia kazi udakaji wa penalti na katika tano hucheza moja hadi mbili.

"Ninafanyia sana mazoezi udakaji wa penalti na nina uhakika kwa zaidi ya asilimia 90, huwezi kunifunga penalti zote tano, lazima nicheze moja ama mbili," alisema kipa huyo wa zamani wa Yanga.

Kwa sasa mashabiki wa Simba, wamekuwa wakipaza sauti zao kwa benchi la ufundi la klabu hiyo, wakitaka Kakolanya kuwa chaguo la kwanza kikosini dhidi ya Aishi Manula.

Kelele zilikuwa nyingi zaidi baada ya Manula kuruhusu mabao mawili kurudishwa kwenye Ligi Kuu dhidi ya Yanga wakati wakimaliza kwa sare ya 2-2, na wengi wakiamini ilitokana na makosa yake.

Habari Kubwa