Matumla amtabiria makubwa Mtango

13Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Matumla amtabiria makubwa Mtango

BONDIA mkongwe nchini, Rashid Matumla amesema bondia, Salum Mtango, ana kiwango kizuri na anaamini ana nafasi ya kutwaa mkanda wa ubingwa wa dunia wa UBO dhidi ya mpinzani wake, Suriya Tatakhun kutoka Thailand.

Mabondia hao wanatarajia kukutana katika pambano la raundi 10 la uzani wa Light litakalofanyika Januari 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini, Tanga.

Akizungumza na gazeti hili jana, Matumla alisema bondia wake alianza mazoezi mapema ili kujiandaa na pambano hilo na anaamini atapeperusha vizuri bendera ya Tanzania.

Matumla alisema hana wasiwasi na maandalizi ya Mtango, na anawaambia mashabiki wa ngumi kwamba mkanda wa pambano hilo utabaki nyumbani.

"Amekuwa akijifua kwa saa sita kila siku, anafanya mazoezi ya kujenga misuli, kutengeneza pumzi, programu hii itakwenda hadi siku mbili kabla ya pambano, anafanya pia mazoezi mepesi akisubiri kupanda ulingoni," alisema Matumla.

Alisema kwa ubora wa Mtango, anaamini ataibuka na ushindi wa Knock Out na hatamaliza raundi 10 zilizopangwa katika pambano hilo.

Mtango aliliambia gazeti hili kuwa amejiandaa kuweka historia ya kuwa bingwa wa dunia na kufuata nyayo za 'kaka' zake akiwamo Matumla ambaye sasa ni kocha wake.

"Nimefanya mazoezi kwa kiwango bora na bado naendelea kufanya mazoezi makali, nahitaji kuweka historia ya ubingwa tena kwa matokeo yasiyokuwa na utata, naamini nitashinda kwa KO," Mtango alisema.

Naye Mratibu wa pambano hilo, Ally Mwanzoa, alisema maandalizi yako katika hatua za mwisho na bondia Tatakhun anatarajiwa kuwasili nchini wiki moja kabla ya pambano.

Mwanzoa alisema kuwa mabondia wote watapima uzito na afya ifikapo Januari 30, mwaka huu jijini Tanga na zoezi hilo litakuwa la wazi.

Aliongeza kutakuwa na mapambano ya utangulizi ambapo bondia Mchanja Bakari atapigana na Sunday Kiwale kwenye uzito wa Light Fly wakati Saidi Mundi atachuana na Mustapha Dotto, huku Adam Yusuph akitarajiwa kucheza dhidi ya Bakari Mohamed, Idrissa Juma atapambana na John Ngotiko pia Mohammed Mutalemwa atazichapa na Simoni Buhura.

Habari Kubwa