Simba: Ni kombe tu

13Jan 2020
Isaac Kijoti
ZANZIBAR
Nipashe
Simba: Ni kombe tu
  • ***Ni marudio ya fainali ya mwaka 2015, Katwila asema ni fainali ngumu ila Mtibwa Sugar itapambana, huku...

TUNATAKA kombe la kwanza mwaka huu wa 2020, hiyo ndiyo kauli ya benchi la ufundi la Simba lililopo chini ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck akisaidiwa na mzawa, Selemani Matola.

Simba na Mtibwa Sugar inayonolewa na Zuberi Katwila, zitashuka katika dimba la Amaan leo kwenye mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Mechi hiyo inayotarajiwa kupigwa kuanzia saa 2:15 usiku ni kama marudio ya fainali ya mwaka 2015 timu hizo zilipokutana na Simba kutwaa ubingwa kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Mtibwa Sugar inashuka dimbani baada ya kuitoa Chipukizi kwa mikwaju ya penalti 4-2 katika hatua ya mtoano kufuatia sare ya bao 1-1 na kisha nusu fainali kuitupa nje Yanga kwa idadi hiyo ya penalti kutokana na sare ya 1-1.

Simba yenyewe, hatua ya mtoano iliichapa Zimamoto mabao 3-1 kisha nusu fainali ikaitoa Azam FC kwa penalti 3-2 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa sare tasa.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven amesema utakuwa mchezo mgumu kwa timu hizo zinazotoka Ligi Kuu Bara kukutana leo, lakini wamejiandaa vema na wanachotaka ni kombe la kwanza mwaka huu.

Aliliambia Nipashe kuwa Mtibwa Sugar ni timu nzuri na inacheza soka la kuvutia, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu kwao kukata tamaa.

"Mechi ya fainali hakuna timu ndogo na Mtibwa wanacheza vizuri, ila tunachotaka ni kombe," alisema.

Mbelgiji huyo alisema anashukuru katika mechi zilizopita hakukujitokeza majeruhi jambo ambalo linampa wigo mpana wa kupanga kikosi chake.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Katwila, akiwa na kumbukumbu ya kulibeba kombe hilo wakati akiwa mchezaji wa timu hiyo mwaka 2010, alisema anafahamu Simba ni timu bora na wamejipanga kwa hilo.

Katwila alisema ukishafika fainali utarajie kukutana na timu bora, lakini si hilo tu anatambua ubora wa Simba mwaka huu hivyo itakuwa mechi ngumu.

"Tumekuja kupambana na tunataka kombe ingawa tunajua mechi itakuwa ngumu kwa kila upande," alisema kocha huyo ambaye mwaka 2010 akiwa mchezaji walilitwaa kombe hilo kwa kuifunga Ocean View katika mchezo wa fainali.

Bingwa wa michuano hiyo mbali na kombe na medali za dhahabu atajinyakulia Sh. milioni 15, huku mshindi wa pili akilamba Sh. milioni 10 na medali za fedha.

Habari Kubwa