Tanzania mwenyeji Kombe la Kagame

13Jan 2020
Somoe Ng'itu
Nipashe
Tanzania mwenyeji Kombe la Kagame

MASHINDANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame mwaka huu yamepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Simba ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Yanga ilimaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita wana nafasi ya kushiriki mashindano hayo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye, alisema uamuzi huo umepitishwa rasmi katika mkutano mkuu wa baraza hilo uliofanyika Desemba mwaka jana.

Musonye ambaye ataachia ngazi nafasi hiyo baadaye mwaka huu alisema mashindano ya Kombe la Chalenji yatafanyika Sudan wakati ya wanawake yatacheza Rwanda pamoja na michuano ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za vijana za wasichana za umri chini ya miaka 17 kwa ukanda huu.

Alisema mashindano ya wanawake ya umri chini ya miaka 20 yatafanyika Uganda wakati yale ya wavulana ya umri chini ya miaka 16 yakipelekwa Djiboiti na Burundi itakuwa mwenyeji wa michuano ya wavulana ya U-20 pamoja na U-17 wasichana.

Aliongeza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Cecafa iliyoko chini ya Rais wa baraza hilo, Wallace Karia, iliteua Kamati ya Mashindano ya watu watano ambao watafanya kazi kwa kushirikiana na Ofisa Mtendaji Mkuu atakayekuja ili kufanya majukumu ya kila siku.

Alimtaja Mwenyekiti wa kamati hiyo atakuwa ni Doris Petra kutoka Kenya na wajumbe wake ni Aimable Habimana (Burundi), Bani Ahmed (Sudan), Justus Mugisha (Uganda) na Eunice Ali wa Djibouti.

Habari Kubwa