Simba, Mtibwa burudani itawale fainali Mapinduzi

13Jan 2020
Mhariri
Nipashe
Simba, Mtibwa burudani itawale fainali Mapinduzi

BAADA ya jana wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla kusherehekea Miaka 56 ya Mapinduzi, leo watahitimisha sherehe hizo kwa kushuhudia mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na Mtibwa Sugar.

Timu hizo zote kutoka Tanzania Bara, zinashuka dimbani baada ya safari ndefu kuanzia hatua ya mtoano, nusu fainali na hatimaye fainali itakayopigwa Uwanja wa Amaan kuanzia saa 2:15 usiku.

Mtibwa Sugar imefika hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti katika mechi zake zote ilizocheza kwenye mashindano hayo mwaka huu.

Ilianza kwa kuitoa Chipukizi kwa penalti 4-2 baada ya sare ya bao 1-1 kwenye hatua ya mtoano kabla ya nusu fainali kuitupa nje Yanga kwa idadi kama hiyo ya penalti kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.

Kwa upande wa Simba, yenyewe ilianza kwa kuitoa Zimamoto kwa mabao 3-1 kabla ya nusu fainali kuitoa Azam FC kwa penalti 3-2 baada ya sare tasa ndani ya dakika 90.

Hivyo, leo timu hizo zitashuka dimbani kila moja ikiwa imejiandaa vema kuweza kupambana na kutwaa ubingwa huo zilioukosa kwa muda mrefu sasa.

Kwa mara ya mwisho Mtibwa kuutwaa ubingwa huo ilikuwa mwaka 2010 ilipotinga fainali dhidi ya Ocean View ya Zanzibar wakati huo kocha wa sasa wa timu hiyo, Zuberi Katwila akiwa mchezaji.

Hivyo, ni dhahiri leo atataka kulibeba kombe hilo ili kuweka rekodi ya kulitwaa na klabu hiyo akiwa mchezaji na hatimaye kocha.

Lakini mchezo wa leo utakumbushia fainali ya mwaka 2015 timu hizo zilipokutana fainali kwenye michuano hii na Simba kuutwaa ubingwa huo kwa ushindi wa penalti 4-3.

Na tangu kipindi hicho, Simba haijawahi tena kulibeba kombe hilo zaidi ya mwaka jana kukaribia kulitwaa, lakini ikajikuta ikilikosa baada ya kufungwa mabao 2-1 na Azam FC katika mechi ya fainali iliyopigwa Uwanja wa Gombani, Pemba.

Hivyo, tunaamini timu zote zimejiandaa kutoa burudani ya kutosha ili kuwafanya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla kuhitimisha sherehe za Mapinduzi kwa furaha na amani.

Aidha, tulishuhudia katika michezo iliyopita kukijitokeza changamoto ya waamuzi kushindwa kumudu mchezo, hivyo tunatoa wito kwa waandaaji wa michuano hii kupanga waamuzi bora na watakaotenda haki kwa kufuata sheria 17 za soka.

Na kwa wachezaji watakaoshuka dimbani leo, tunataka kuona wakicheza soka la kiungwana zaidi na kuepuka rafu ambazo zinaweza kusababishiana majeraha yatakayowaweka benchi kwenye mechi zijazo za Ligi Kuu Bara.

Tunatambua baada ya mechi hii ya fainali timu zitarejea kwenye Ligi Kuu, hivyo Nipashe tunatamani kuona wachezaji wakionyesha viwango na burudani zaidi na si vita vya kuumizana. Tunazitakia fainali njema Simba, Mtibwa.

Habari Kubwa