Mwanasoka hadharau hata Kombe la Mbuzi

13Jan 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Mwanasoka hadharau hata Kombe la Mbuzi

"HAYA ni mashindano ambayo tulikuwa makini na wachezaji wetu wasipate majeraha, ili tukirudi kule kwenye ligi tuwe na nguvu zaidi." Ni baadhi ya maneno ya Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz-

-akizungumza kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar baada ya timu yao kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar.

Ameongea maneno mengi, lakini leo naangalia maneno yake haya ambayo amejaribu kuyazungumza, nadhani kuwapoza mashabiki wa Yanga wachukulie kama viongozi hao na benchi lao la ufundi hawakuwa wakiyatolea macho mashindano hayo.

Kuna baadhi ya mashabiki walikwenda mbali sana na kusema kuwa ofisa huyo ameyadharau mashindano hayo ambayo yana heshima kubwa Zanzibar, kwani yanafanyika wakati wa kumbukumbu ya Mapinduzi ya kisiwa hicho kila mwaka.

Kwangu mimi sidhani kama Nugaz ameyadharau la hasha. Ila amefanya hivyo kuwapoza tu baadhi ya wanachama na mashabiki wa Yanga kuonyesha kuwa hawakuwa na mpango na michuano hiyo na akili yao iko kwenye Ligi Kuu Bara.

Simwambii Nugaz, tu, bali wanamichezo wote ambao wana fikra kuwa michuano pekee muhimu ni ligi basi atakuwa anakosea na ninakuwa na wasiwasi na uanamichezo wake.

Michezo ni michezo tu. Ndiyo maana hata uswahilini klabu zinaingia kwenye michuano ya kugombea mbuzi tu, lakini zinakodisha wachezaji mpaka wa Ligi Kuu kwa gharama kubwa.

Pesa anayolipwa mchezaji mmoja wa Ligi Kuu, unaweza kununua hata mbuzi watatu.

Klabu inakodisha wachezaji hata watano mpaka sita wa Ligi Kuu na michuano inaendeshwa wakati mwingine mwezi mzima, timu inayofika fainali na kuchukua mbuzi inaweza kucheza hata mechi sita mpaka nane, inaingia gharama za chakula kwa wachezaji, usafiri na maandalizi mengine ya mechi, lakini inakuja kuambulia mbuzi mmoja tu. Tena utakuta viongozi wa klabu na mashabiki wao wanafurahi na kuweka rusha roho ambalo nalo wanaingia gharama, na kununua mchele kwa ajili ya sherehe za kumtwaa mbuzi. Kwa nini wanafanya hivyo? Kwa nini waingia gharama kubwa kwa sababu ya mbuzi tu? Lengo hapo si mbuzi, ila wana moyo wa uanamichezo.

Mwanamichezo wa ukweli hadharau kombe, au michuano yoyote na wala hawezi kuwaambia wachezaji wasikaze kwa sababu ni michuano midogo.

Kama suala ni majeruhi, ni kwamba mchezaji anaweza kupata kuwa majeruhi hata kwenye mazoezi na si kwenye michuano ya Mapinduzi tu.

Ninavyojua klabu, kocha au mchezaji huwa wanaangaliwa thamani kwa kuchukua mataji na haijalishi ni ligi, FA au michuano mingine mbalimbali, yote inahesabika na kuingia kwenye wasifu.

Ndiyo maana tunaona hata Ulaya, timu zinacheza michuano mingi kama Ligi ya Mabingwa, Europa, ligi ya ndani, Komba la FA na mengine kama Ngao ya Jamii ambayo makocha na wachezaji huchukulia kwa uzito ule ule na pia huyaheshimu na kuyahesabu wanapoyatia kwenye makabati yao.

Hapa kwetu tu ndiyo kuna baadhi ya watu ambao wao wanachoonekana kuheshimu ni Ligi Kuu tu, kwa sababu eti ndilo linalotoa mwakilishi wa kwenda kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ikumbukwe kuwa bingwa wa ligi ni mmoja tu, klabu au kiongozi anayeonekana anadharau michuano mingine, akikosa ubingwa ina maana kaisababisha timu yake ikose taji lolote kwa msimu huo.

Yanga ilianzishwa mwaka 1935 na Simba 1936, Ligi Kuu ilianzishwa mwaka 1965, hii ina maana kuwa klabu hizo kabla ya ligi ilikuwa ikicheza michuano au vikombe vingine mbalimbali nchini.

Hapa ndipo inapoonyesha kuwa viongozi wa klabu hizi zamani na zingine zilizokuwapo walikuwa ni wanamichezo wa kweli kwa sababu hawakudharau michuano hiyo na hata Ligi Kuu ilipoanzishwa bado kulikuwa na vikombe vingi kama Kombe la Hedex, Kombe la CCM, Kombe la Nyerere, Kombe la Jengo, Kombe la Ofuma na mengine mengi, kila timu ikija na kikosi kamili wakati mwingine Simba na Yanga zikikutana fainali.

Hii ya kudharau michuano siku hizi na kusema kuwa wachezaji wataumia inatoka wapi?

Habari Kubwa