Harerimana atangazwa rasmi kocha mpya KMC

14Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Harerimana atangazwa rasmi kocha mpya KMC

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Lipuli FC ya Iringa, Haruna Harerimana, ametangazwa rasmi kujiunga na timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, KMC FC ya jijini Dar es Salaam.

Harerimana ametua KMC kuchukua nafasi ya Mganda Jackson Mayanja ambaye mkataba wake ulisitishwa kutokana na timu hiyo kutokuwa na mwenendo mzuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa waliyoshiriki.

Mwenyekiti wa Bodi ya KMC, Benjamin Sitta, alisema jana jijini kuwa uongozi wa klabu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni umeingia mkataba wa miezi 18 na kocha huyo baada ya kukidhi vigezo walivyoviweka.

Sitta alisema kuwa Harerimana amepitishwa na bodi ya timu ambayo ilipitia maombi kutoka kwa makocha mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania walioomba kuchukua nafasi iliyoachwa na Mayanja.

"Mchakati wa kutafuta kocha haukuwa rahisi kutokana na ujuzi na uzoefu wa makocha waliomba kuchukua nafasi ya Mayanja, ambayo ilishikiliwa kwa muda na Kaimu Kocha Mkuu, Hamadi Ally," alisema Sitta.

Alisema tayari Harerimana ametambulishwa kwa wachezaji na ameanza kazi ya kuinoa KMC kwa ajili ya kusaka matokeo mazuri katika Ligi Kuu na mashindano ya Kombe la FA.

“Ni kocha ambaye amekidhi vigezo vyote ambavyo tumeweka na uongozi kuamua kuingia naye mkataba. Kupitia yeye, tunaamini timu itafanya vema na kurejesha ubora wake wa msimu uliopita,” alisema Sitta.

Harerimana alisema amekuja kufanya kazi na kama ilivyo makocha wengi duniani, amejipanga kuipa mafanikio.

“Nimekuja kufanya kazi yenye mafanikio, hivyo naomba wachezaji tushirikiane katika kuleta matokeo chanya ya timu na kumaliza ligi katika nafasi nzuri. Nimefurahi kupata uongozi ambao unajali maslahi ya wachezaji na watendaji wa timu,” alisema Harerimana.

Wakati huo huo, KMC imefikia makubaliano ya kuachana na wachezaji watano kutokana na sababu mbalimbali.

Wachezaji hao ni pamoja na Aaron Lulambo, George Sangija, Rehani Kibingu, Melly Mongolare na Janvier Besala Bokongu.

Habari Kubwa