Shime afunguka kazi haijamalizika

14Jan 2020
Shufaa Lyimo
Nipashe
Shime afunguka kazi haijamalizika

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wasichana ya umri chini ya miaka 17, Bakari Shime amewataka Watanzania wazidi kuisapoti timu hiyo huku akisema kazi bado haijamalizika.

Beki wa Timu ya Taifa ya Vijana ya Wasichana wa umri chini ya miaka 17, Protasia Mbunda (kulia), akiwania mpira dhidi ya beki wa Burundi, Annonciatte Nshimirimana katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam juzi. PICHA: JUMANNE JUMA

Tanzania juzi ilianza vema kampeni ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa kuifunga Burundi magoli 5-1.

Akizungumza na gazeti hili jana, Shime alisema ushindi huo umetokana na wachezaji wake walifuata maelekezo na anaamini wataendelea na kasi hiyo katika mchezo wa marudiano.

Alisema hata hivyo wapinzani wao wameonyesha kiwango kizuri na waliingia katika mchezo huo kwa kutowadharau kutokana na kukumbuka sare ya mabao 3-3, waliyoipata mara ya mwisho walipokutana.

"Wachezaji wangu wamenifurahisha kwa sababu wamefanya niliyokuwa nayataka kuhakikisha wanaipeperusha vema bendera ya Taifa," alisema Shime.

Alisema amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano na wataendelea kujiimarisha ili wafanye vema katika mchezo wa marudiano.

"Nawashukuru Watanzania kwa sapoti waliyotuonyesha kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kushuhudia kazi inayofanywa na mashujaa wao," Shime alisema.

Naye beki wa timu hiyo, Protasia Mbunda, alisema wanashukuru Mungu kwa matokeo mazuri waliyoyapata licha ya mchezo huo kuwa mgumu.

Mbunda alisema siri ya mafanikio ni kumsikiliza mwalimu wao kwa makini na kufuata maelekezo anayowapa.

"Tunashukuru kwa matokeo tuliyoyapata, mchezo ulikuwa mgumu, lakini tumejitahidi mpaka tumepata ushindi," alisema nyota huyo ambaye alifunga bao moja.

Mabao mengine katika mechi hiyo yalifungwa na Joyce Meshack na Aisha Masaka ambaye alifunga hat-trick.

Timu hizo zinatarajia kurudiana Januari 25, mwaka huu mjini Bujumbura.

Habari Kubwa