Tiketi mabasi yote kiektroniki

14Jan 2020
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Tiketi mabasi yote kiektroniki

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), kinatarajia kuanza kukatisha tiketi kwa njia ya kielektroniki mwezi ujao kwa kampuni zote za mabasi, ili kupunguza msongamano unaojitokeza.

Vilevile, Taboa imesema inatekeleza agizo la Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, kuhusu kuzingatia leseni zao katika usafirishaji wa vipeto kwenye mabasi.

Katibu wa chama hicho, Enea Mruto, katika mazungumzo na Nipashe jijini Dodoma jana, alisema baada ya kikao chao na Mamlaka ya Mapato (TRA), wamekubaliana ukatishaji tiketi ufanyike kwa njia ya elektroniki kuanzia mwezi ujao kwa mabasi yote.

"Kama TRA hawatatuangusha kile tulichokubaliana nao, basi mpango huo utaanza rasmi mwezi ujao, tunahitaji kufanya kazi kwa kwenda na teknolojia mpya," alitamba.

Alisema utaratibu huo ulioanza katika baadhi ya kampuni za mabasi, utatumika kwa kampuni zote za mabasi baada ya kukamilika kwa baadhi ya mambo waliyokubaliana kisha utazinduliwa rasmi na kuwekwa agizo kwa mabasi yote.

Alisema mfumo huo utasaidia kuwarahisishia wateja kupata tiketi au kuweka maombi ya kukata tiketi kwa njia ya mtandao.

"Unajua mambo sasa hivi yanakwenda kisasa zaidi, hivyo na sisi tunahitaji kwenda kiteknolojia," alisema na kukiri kuwa tayari kuna kampuni chache za mabasi nchini zimeujaribu utaratibu huo.

Kuhusu zuio la Nditiye kwa mabasi kusafirisha baadhi ya nyaraka, Mruto alisema Taboa inatekeleza agizo kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa kwenye leseni zao za usafirishaji wa vipeto.

Alisema hata katika mkutano wao uliopita, wamiliki walisisitiza agizo hilo ili kuendana na sheria zinavyotaka.

"Taboa tunatekeleza agizo hilo, atakayekiuka atakupambana na mkono wa sheria, hivyo kila mmoja anapaswa kutekeleza sheria," alionya.

Mruto pia alisema Taboa imeweka mikakati mingi ya kuboresha huduma zake na kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua nchini kwa kuhimiza umakini katika kampuni za mabasi, hasa kwa madereva.

Alisema chama hicho kitakuwa kinasisitiza wamiliki wa mabasi kufanya ukaguzi katika vyombo vyao vya moto mara kwa mara ili kuepusha ajali.

Habari Kubwa