Maelfu wamiminika kusajili laini za simu

14Jan 2020
Salome Kitomari
Nipashe
Maelfu wamiminika kusajili laini za simu

ZIKIWA zimebaki siku sita, idadi ya wanaosajili laini za simu kwa mfumo wa alama za vidole inaongezeka.

Akizungumza jana na Nipashe, Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala, alisema hadi Januari 7, mwaka huu jumla ya laini 25,160,147 zilisajiliwa ikiwa ni asilimia 42.42.

Aidha, alisema  jumla ya laini 22,796,472 hazijasajiliwa, na kuwataka wananchi kutumia vyema siku zilizosalia kukamilisha usajil wao.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, ambao hawajasajili laini zao ni asilimia 47.5.

“Mwamko wa wananchi kujisajili unazidi kukua kadri siku zinavyokwenda, ndiyo maana kunaongezeko la usajili,” alisema na kuongeza:

“Usajili huu ni muhimu sana kuwalinda wananchi dhidi ya wizi, ulaghai, utapeli na uchochezi.”

Kwa mujibu wa Mwakyanjala, kuna jumla ya laini 47,956,619.

Awali, mwisho wa usajili ulikuwa ni Desemba 31, mwaka jana, lakini Desemba 27, Rais John Magufuli wakati anasajili laini yake kwa alama za vidole wilayani Chato, mkoani Geita, aliongeza siku 20 hadi Januari 20, mwaka huu.

Habari Kubwa