Upelelezi kesi ya Kabendera wanukia

14Jan 2020
Hellen Mwango
Nipashe
Upelelezi kesi ya Kabendera wanukia

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili  mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera, umedai kuwa bado kuna maeneo machache wanayafanyia kazi kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.

Madai hayo yalitolewa na Wakili wa Serikali mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega.

Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 27, mwaka huu  itakapotajwa, na kuamuru mshtakiwa aendelee kukaa mahabusu.

Kabendera anadaiwa  kupanga na kushirikiana na genge la uhalifu na shtaka la tatu ni la kukwepa kodi zaidi ya  Sh. milioni 173.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa  siku na mahali pasipofahamika   mshtakiwa alijihusisha na genge la uhalifu.

Alidai kuwa katika tarehe tofauti tofauti kati ya Januari mwaka 2015 na Julai mwaka 2019, alitenda kosa la kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia maslahi.

Katika shtaka la pili, Kabendera anakabiliwa na shtaka la ukwepaji kodi, zaidi ya Sh. 173,247,047.02.

Kabendera anadaiwa kuwa katika tarehe tofauti tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 19, 2019, alishindwa kulipa kodi kiasi cha Sh. 173,247,047,02.

Katika shtaka la tatu, Kabendera anadaiwa kati ya Januari 2015 na Julai 2019, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, alitakatisha fedha kiasi cha Sh. 173,247,047.02.

Habari Kubwa