Waziri aagiza meli iliyokamatwa uvuvi haramu itolewe bandarini

14Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
MTWARA
Nipashe
Waziri aagiza meli iliyokamatwa uvuvi haramu itolewe bandarini

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amemtaka Mmiliki wa Meli ya Buah Naga 1, iliyokamatwa kwa makosa ya uvuvi haramu katika ukanda wa Bahari Kuu, kuiondoa haraka meli hiyo kwenye Bandari ya Mtwara, ili kupisha shughuli zingine za serikali.

Amesema meli hiyo inapaswa kuondolewa bandarini huko kwa kuwa tayari mahakama ilishatoa hukumu dhidi ya kesi hiyo.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo iliko meli hiyo inayomilikiwa na raia wa Malaysia, Waziri Mpina alisema jana kuwa kukamatwa kwa meli hiyo na kisha mahakama kutoa hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh. bilioni moja, ni uthibitisho kuwa serikali ya awamu ya tano haina mzaha katika kusimamia rasilimali zake, zikiwamo za uvuvi.

Waziri huyo alisema meli hiyo ni ya pili kukamatwa na kuchukuliwa hatua na serikali, kutokana na kufanya uvuvi haramu katika Bahari Kuu ndani ya miaka 10, ya kwanza ikiwa ni Tawariq 1, iliyokamatwa mwaka 2009 na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. John Magufuli, sasa Rais wa Tanzania.

Mpina alisema baada ya Dk. Magufuli kukamata meli hiyo miaka 10, baadaye, serikali anayoiongoza imekamata tena meli nyingine na kuitangazia dunia kuwa Tanzania imekataa kuwa shamba la bibi la kila mtu kuja kufanya anachotaka.

Alisema adhabu iliyotolewa na mahakama inatoa fundisho na ujumbe kwa wamiliki wa meli na vyombo vingine vinavyotumika kufanya shughuli za uvuvi, kuzingatia sheria za nchi.

Waziri huyo alisema serikali itaendelea kufanya doria na operesheni katika ukanda wa Bahari Kuu na kudhibiti meli zote za kigeni zilizotumika kuvua katika maji ya Tanzania bila kufuata sheria.

Alisema uvuvi huo usiozingatia sheria za nchi, si endelevu kutokana na wavuvi kuvua papa na kisha kutupa miili yao baharini baada ya kuondoa mapezi.

Desemba 2018, Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa Kanda ya Mtwara, iliwahukumu watu watatu wakiwamo raia wawili wa kigeni na Mtanzania mmoja, kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja au kulipa faini ya Sh. bilioni moja baada ya kukamatwa wakifanya uvuvi haramu katika ukanda wa Bahari Kuu Januari mwaka huo.

Watu hao walikamatwa katika ‘Operesheni NMATT’, iliyokuwa inaendeshwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola.

Watu hao walikamatwa wakiwa kwenye meli ya Buah Naga 1 ya Malaysia wakiwa na kilo 90 za mapezi ya papa bila kuwa na miili yake, kinyume cha sheria.

Pia mwishoni mwa mwaka jana, Bunge la Tanzania lilipitisha Azimio la Mkataba wa Kimataifa wa Shirika la Chakula Duniani wa kupambana na kuzuia uvuvi haramu kupitia bandari za nchi wanachama, Spika Job Ndugai akitaka juhudi zaidi kufanyika kulinda rasilimali za uvuvi akisisitiza kuwa endapo hazitasimamiwa vizuri, zitatoweka.

Habari Kubwa