Ajali ya basi ilivyoua wawili

14Jan 2020
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Ajali ya basi ilivyoua wawili

WATU wawili wamefariki dunia, huku saba wakijeruhiwa ajali ya basi lenye namba za usajili T 437 DFJ Bright Line, wakati likitokea Mwanza kwenda Dodoma kugongana uso kwa uso na gari dogo.

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya asubuhi katika Kijiji cha Isela Kata ya Samuye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Imeelezwa kuwa basi hilo lilipofika eneo hilo lilikutana na mwendesha bodaboda katikati ya barabara na kumkwepa, ndipo likakutana uso kwa uso na gari ndogo lenye namba za usajili T 173 ANW na kusababisha ajali.

Akisimulia, abiria aliyenusurika kwenye ajali hiyo, Matei Onyango, alisema walipofika kwenye kijiji hicho wakati basi likiwa katika mwendo wa kawaida, wakashangaa kuona linaanza kuyumba walipo angalia mbele kujua kuna nini, ndipo wakaona kofia ya mwendesha bodaboda imerushwa juu kisha wakagongana na gari ndogo.

“Mimi ni mkazi wa Rorya mkoani Mara,  napeleka watoto wangu wawili shuleni Igunga, nikiwa ndani ya basi hili nikiangalia video ya wanyama, tulipofika eneo hili nikaanza kuona basi linayumba, kutizama mbele nikaona kofia ya mwendesha boda imerushwa juu, kidogo nikasikia kishindo kikubwa cha kugongana na gari dogo, ndipo tukapata ajali,” alisema Onyango.

“Namshukuru Mungu mimi na watoto wangu wawili tumetoka salama licha ya kupata majeraha madogo, lakini kama dereva angekuwa kwenye mwendo kasi sidhani kama tungesalimika… ajali ni mbaya sana ukiona hata namna tulivyoanguka,” aliongeza.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Shinyanga, Athony Gwandu, ambaye alikuwapo eneo la tukio, aliwataja watu wawili waliofariki papo hapo kwenye ajali ni Paulina Obedi (12) ambaye ni abiria, na mwendesha bodaboda aliyefahamika kwa jina moja na Saidi, mkazi wa Kijiji cha Busongwa Shinyanga Vijijini.

Alisema majeruhi hao saba walikimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, na wanapatiwa matibabu, huku abiria wengine waliosalimika waliwasafirisha kwenye basi lingine na wanaendelea na safari.

Gwandu alifafanua kuwa basi hilo lilikuwa na abiria 55.

Alitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni dereva wa basi hilo kujaribu kumkwepa mwendesha bodaboda, ndipo alipokutana uso kwa uso na gari jingine dogo na kugongana uso kwa uso, na kuwataka madereva wote wa vyombo vya moto wakiwamo bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali.

Habari Kubwa