Majaliwa ‘aiamsha’ Takukuru uchunguzi wizi fedha korosho

14Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa ‘aiamsha’ Takukuru uchunguzi wizi fedha korosho

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ukamilishe mapema uchunguzi dhidi ya madudu yaliyoibuliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 na wizi uliofanywa na viongozi wa AMCOS kwa wakulima wa ufuta na korosho ikiwamo Wilaya ya Ruangwa.

Aliyasema hayo jana wakati akizindua jengo la Takukuru Wilaya ya Ruangwa lililogharimu zaidi ya Sh. milioni 142. Alitoa wito kwa Takukuru kuwa imara na kutembea kifua mbele katika mapambano hayo. 

Alisema pamoja na Takukuru kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, na ameuagiza uongozi wa taasisi hiyo ukamilishe mapema utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Rais John Magufuli aliyoyatoa kwao kwa nyakati tofauti.

Alisema ameshuhudia kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya kupitia uchunguzi na ufuatiliaji wa madai ya malipo ya wakulima wa zao la ufuta na korosho.

“Kamilisheni chunguzi hizi zote kwa wakati ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliopatikana na hatia.”

Alisema rushwa huathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Kutokana na ukweli huo, serikali imetoa msukumo wa pekee katika kushughulikia vitendo vya rushwa na ufisadi. Msukumo huo, umechangia kwa kiasi kikubwa hususan katika kipindi hiki, utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati kwa ufanisi na kwa wakati.” 

Alisema wananchi wanatakiwa wafahamu kwamba nchi yoyote ambayo rushwa imetamalaki siyo rahisi kuwa na uwezo wa kiuchumi utakaoiwezesha nchi hiyo kumudu kulipa madeni ya ndani na ya nje. “Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania tunashuhudia jinsi Serikali ya awamu ya tano inavyolipa madeni.” 

Kwa mfano, kati ya Julai na Septemba, 2019, Sh. bilioni 85.72 zimetolewa ikiwamo bilioni 50 za madai ya pensheni; bilioni 22 za madai ya watumishi wa umma ikiwamo kiinua mgongo kwa wastaafu 3,019 na malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 1,435; bilioni 10.24 zimelipa watoa huduma na zaidi ya bilioni 2 kwa ajili ya makandarasi na wahandisi washauri. Hayo ni matokeo ya jitihada za kupambana na rushwa zinazofanywa na serikali.

Alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuwa ikijipambanua na vita dhidi ya rushwa na ufisadi. Hivyo, kitendo hicho cha kuendelea kulipa madeni ni ishara ya mafanikio ya serikali katika jitihada zake za kuzuia na kupambana na rushwa nchini, na kuwa serikali itaendelea kudhibiti mianya yote ya rushwa katika utendaji mzima wa serikali.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema tafiti za hivi karibuni zilizofanywa na wadau wa mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora kama vile Transparency International (TI), MO Ibrahim na Afro barometer zinaonyesha kuwa kwa miaka mitatu mfululizo, yaani 2016 hadi 2018 Tanzania imeendelea kufanya vyema katika mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora. 

Alisema mafanikio hayo ya kujivunia ni jitihada za serikali za kusimamia kwa dhati mapambano dhidi ya rushwa kwa usimamizi wa Takukuru ambayo ndicho chombo kilichopewa dhamana kisheria. 

“Tambueni kwamba uongozi mzima wa juu kabisa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu) uko pamoja nanyi katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi,” alisema. 

Pia ameagiza kuanzishwa kwa vilabu vya kupambana na rushwa katika shule ili wanafunzi waweze kuwa na uelewa na kuweza kutoa taarifa za rushwa. 

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema jengo hilo limejengwa kwa miezi saba kuanzia tarehe Juni 11, 2018 na kukamilika Januari 25, mwaka jana, na kuwa hadi kufikia hatua ya uzinduzi, limegharimu Sh. 142,857,142.86.

Kuhusu uchunguzi, alisema kwa kipindi cha mwaka 2019 Takukuru imefanya uchunguzi kwenye tuhuma kubwa ikiwamo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Magufuli aliyoyatoa Oktoba 15, 2019 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Ruangwa.

“Kupitia uchunguzi ule, tumebaini kwamba zaidi ya vyama 30 vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vya Mkoani Lindi viliwadhulumu wakulima wa  ufuta kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni Sh. 1.23.  Kupitia uchunguzi huo tuliwakamata na kuwahoji zaidi ya viongozi 300 wa AMCOS zilizokuwa zinahusika katika dhuluma hii. Tulifanikiwa kuokoa zaidi ya Sh. bilioni 1.042. Fedha hizi zilikuwa ni mali ya wakulima wa ufuta ambao walidhulumiwa fedha hiyo na Viongozi wa Vyama vya AMCOS.”

Habari Kubwa