Mitambo ya mabilioni yatua kwa Mkemia Mkuu serikalini

14Jan 2020
Mary Geofrey
Nipashe
Mitambo ya mabilioni yatua kwa Mkemia Mkuu serikalini

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imenunua mitambo tisa yenye thamani ya Sh. bilioni 6.5 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli, kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa mamlaka hiyo.

Kutokana na kuwapo kwa mitambo hiyo ya kisasa, mamlaka hiyo imepunguza siku za kupima vinasaba na kutoa majibu kutoka ndani ya siku 21 ilivyokuwa awali hadi siku moja kwa sasa.

Mafanikio hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, alipozungumza na waandishi wa habari na maofisa mawasiliano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, waliotembelea mamlaka hiyo.

"Uwekezaji huu wa mitambo ya kisasa umeongeza kasi na uwezo wa GCLA kufanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali, zikiwamo za dawa za kulevya, uchunguzi wa mazingira, vinasaba vya binadamu na wanyama na ubora wa chakula," alisifu.

Alisema kuwapo kwa mitambo hiyo ya kisasa pia kumesaidia kutoa huduma kwa wingi na kwa kasi kulinganisha na miaka ya nyuma.

Alisema mamlaka hiyo pia imefanikiwa kukarabati miundombinu ya ofisi zote za kanda nchini kwa gharama ya Sh. bilioni 1.3, hivyo kusaidia kuboresha utendaji kazi.

Dk. Mafumiko alisema katika kipindi hicho, pia walifanikiwa kusajili wadau wa kemikali 2,426 na vibali 21,336 na kufanya kazi katika mipaka yote na katika bandari nchini kwa saa 24.

Habari Kubwa