CCM yashtukia vikumbo uchaguzi ubunge, udiwani

14Jan 2020
Jumbe Ismaily
MANYONI
Nipashe
CCM yashtukia vikumbo uchaguzi ubunge, udiwani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewashtukia makada wake kadhaa wanaodaiwa kupigana vikumbo kujipitisha kwa wanachama kama sehemu ya maandalizi ya kugombea nafasi mbalimbali ukiwamo udiwani na ubunge mwaka huu.

Hata hivyo, hatua hiyo inakiuka maelekezo ya chama hicho tawala, ambayo yanawakataza kujihusisha kwa namna yoyote na kampeni za uchaguzi mkuu.

Viongozi wakuu wa chama hicho, hususan Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Philip Mangula, mara kwa mara amekuwa akitoa angalizo kuwa watakaokaidi, majina yao yatakakwa kama ilivyofanyika mwaka 2015. 

Wakati hali ikiwa hivyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, Jumanne Makhanda, amewashtukia baadhi ya makada wanaojipitisha kwa wanachama, ikiwapo kuwapa rushwa kama njia ya kuwashawishi wawaunge mkono.

Kutokana na hali hiyo, Makhanda amewatahadharisha wote wanaojipitisha pitisha kwa ajili ya kuanza ushawishi, kuwa watashughulikiwa. Aidha, amesema wapo wanaotoa rushwa ya kati ya Sh. 20,000 hadi Sh. 30,000.

Mwenyekiti huyo alitoa agizo hilo kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya hiyo, kilichokutana kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa mwaka 2015-2020 iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa.

Aidha, alisema baadhi ya wanachama wanaodhamiria kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao, wanatakiwa kutoanza kampeni kabla ya wakati.

Mwenyekiti huyo alisema chama hicho hakitasita kukata majina ya wagombea watakaogundulika kuanza kampeni hizo kabla ya wakati.

Kwa mujibu wa Makhanda, wilayani humo wameanza kujitokeza baadhi ya watu wenye nia ya kugombea, kuanza kupitapita na kutoa rushwa kwa wananchi, na kwamba kuna baadhi ya viongozi wamegeuka kuwa  madalali wa wagombea hao, jambo ambalo halikubaliki kikanuni.

Alisema wote wenye nia ya namna hiyo hawana nafasi, na hawatakuwa na nafasi hiyo kwa sasa kwani waliopo madarakani wanafanyakazi na ndiyo wanaoitumikia ilani ya CCM.

“Na natumia nafasi hii kwenye vyombo hivi vya habari kupiga marufuku watu wote wenye nia ya kugombea nafasi ya kuanzia nafasi ya urais, ubunge na udiwani hawana nafasi. Waliopo wanafanyakazi na ndiyo wanaitumikia ilani ya chama,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.

Alisema atakuwa mkali kwa kuhakikisha analisimamia kwa karibu jambo hilo.

Kadhalika, aliwaonya baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaojigeuza kuwa madalali wa kuwachagulia wananchi viongozi kwa kuwarubuni wananchi kwa kuwahonga fedha.

Alihoji kuwa anayetoa fedha hizo alizogawa kwa wapigakura atakapochaguliwa atazirudishaje, na kuwa jambo hilo linalotia shaka.

“Wewe unapotoa kati ya Sh. 20,000 au 30,000 unategemea uje upewe  huo uongozi, ili kusudi ukalipe nini, hii hela utakuja kuilipaje, kwanza unaipata wapi kama siyo utapeli unaowafanyia wananchi?

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Chama kilishaweka bayana kwamba kipindi cha kuwachagulia wananchi viongozi kimepitwa na wakati, na kwamba kiongozi yeyote wa chama ni lazima akachaguliwe na wanachama muda utakapofika.

Wakati Makhanda, akishtukia kampeni zisizo rasmi na kutoa angalizo, takribani wiki moja iliyopita CCM Mkoa wa Mara, ilitoa angalizo kama hilo, baada ya kubaini baadhi ya makada kuanza kampeni kabla ya muda.

Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Samuel Kiboye, ndiye aliyetoa angalizo hilo kwa makada wanaovunja kanuni za chama kwa kuanza kutangaza nia kabla ya wakati, na kwamba watashughulikiwa kwa kuwa wanahujumu waliopo madarakani.

Habari Kubwa