Yanga, Kagera tambo zatawala

14Jan 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga, Kagera tambo zatawala
  • ***Ni kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho jijini...

WAKATI uongozi wa Yanga jana uliwapa rasmi mikataba makocha wake wapya, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, ametamba timu yake itapata matokeo mazuri katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla (wa pili kushoto), akionyesha nakala ya mkataba wa kazi baada ya Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Luc Eymael (kulia) na Kocha wa Viungo, Riedoh Berdien (kushoto) jana, kutua jijini Dar es Salaam. PICHA: YANGA SC

Makocha wa Yanga waliopewa mkataba wa miezi 18 kila mmoja ni Kocha Mkuu Mbelgiji Luc Eymael na Msaidizi wake, Riedoh Berdien ambaye ni Kocha wa Mazoezi ya Utimamu wa mwili.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli aliliambia gazeti hili jana wamekamilisha mazungumzo na makocha hao na wana imani wataipa mafanikio klabu yao.

"Kile kitu kimekamilika, Luc Eymael na Riedoh Berdien ni mali yetu (Yanga) hadi Juni mwaka 2021, karibuni sana tuijenge Yanga," alisema kwa kifupi Bumbuli.

Kiongozi huyo alisema kikosi chao kimekamilika na sasa wamejipanga kuendeleza ushindi katika ligi hiyo ambayo ubingwa wake unashikiliwa na watani zao.

"Kwa sasa tuko vizuri kila idara, tulitumia muda wa dirisha dogo kujiimarisha, tunawaomba mashabiki na wanachama wetu wasiwe na wasiwasi, Yanga iko imara na imedhamiria kurejesha heshima," Bumbuli alisema.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, amesema kikosi chake kimejiandaa kuweka rekodi mpya ya kupata pointi tatu dhidi ya Yanga .

Maxime alisema wachezaji wake wako katika hali nzuri na leo asubuhi wanatarajia kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Kawe ili kuhakikisha wanaingia uwanjani wakiwa na ari ya ushindi.

"Wamekuwa wakinisumbua sana, ila msimu huu nimejiandaa kuvunja mwiko, tangu nimekuwa na Kagera Sugar sijawafunga, ila mechi ya keshokutwa (kesho), watashangaa," alisema Maxime.

Aliongeza kuwa kiufundi wachezaji wake wanauwezo wa kupata ushindi na anachohitaji ni kuona wanaongeza utulivu wanapokuwa na mipira.

"Kama tutaamka vema, nina uhakika tutapata pointi tatu, mazoezi ya mwisho tutafanya kesho (leo) asubuhi, nitapata picha ya nani ataanza na nani ataanzia benchi," aliongeza nahodha huyo wa zamani wa Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Baada ya mechi hiyo ya keshokutwa, Yanga itaendelea kujiimarisha kwa ajili ya kukutana na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Habari Kubwa