Simba yaifuata Mbao mapema

14Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simba yaifuata Mbao mapema

KIKOSI cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kinatarajiwa kuwasili jijini Mwanza leo tayari kuwavaa wenyeji Mbao FC katika mechi ya ligi hiyo itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, imeelezwa.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, aliliambia gazeti hili jana kikosi hicho kimeamua kwenda mapema jijini humo ili kuwapa nafasi ya kupumzika wachezaji wao ambao wametoka katika fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Rweyemamu alisema hakuna mchezaji ambaye ni majeruhi, benchi la ufundi limedhamiria kuona wachezaji wanapambana katika kila mchezo ulioko mbele yao.

"Tutaondoka Zanzibar kesho (leo) na tutaunganisha moja kwa moja kuelekea Mwanza kesho (leo) hiyo hiyo, hatutakuwa na kituo Dar es Salaam, ukiiangalia ratiba haionyeshi nafasi ya kupumua, tutapumzikia huko huko," Rweyemamu alisema.

Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 35 baada ya kucheza mechi 14, watabakia jijini huko kwa ajili ya mechi nyingine dhidi ya Alliance FC itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Ndanda FC ya Mtwara yenye pointi tisa na imeshuka dimbani mara 17 ndio inaburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20 na ambayo itateremka klabu sita msimu huu.

Habari Kubwa