Wafugaji ng'ombe wapewa neno

15Jan 2020
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe
Wafugaji ng'ombe wapewa neno

DAKTARI Bingwa wa Mifugo Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Safan Kagome, amewataka wafugaji wa ng'ombe kuchanja mifugo yao, ili kuwakinga dhid ya ugonjwa wa vipele unaosumbua kwa sasa baada ya kutoweka mwaka 2015.

"Kila ng'ombe chanjo itatolewa kwa Sh. 400 tu, hivyo kila mmoja ni vyema akapeleka ng'ombe wake ili aepukane na ugonjwa huo," alishauri.

Dk. Kagome alikuwa anazungumza na wenyeviti na watendaji wa vijiji vya wilaya hiyon kwenye Ukumbi wa Halmashauri, akibainisha kuwa chanjo hiyo inaanza kutolewa Januari leo.

Alisema awali walikubaliana tarehe hiyo, ila baadhi ya maeneo wilayani hapo yaliomba kutolewa kabla ya tarehe tajwa, hivyo Kijiji cha Tingatinga kilichoko Tarafa ya Enduiment, chanjo hiyo ilitolewa Januari 9 mwaka huu.

Dk. Kagome alisema wilaya hiyo inakadiriwa kuwa na ng'ombe zaidi ya 200,000 na kuwaagiza wafugaji hao, kuhakikisha mifugo hiyo inapata chanjo.

"Sheria ya Mifugo inasema kila mfugaji lazima achanje mifugo yake na asiyechanja, lazima ashtakiwe mahakamani, adhabu yake ni faini kuanzia Sh. 300,000 au 500,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela. Hata ikiwezekana adhabu zote kwa pamoja," alionya.

Pia, aliwataka viongozi hao kufufua majosho yaliyoko katika maeneo yao, kwa kuwa serikali imetoa dawa aina ya Parinet lita 136 kwa ajili ya kuogesha mifugo ili kudhibiti kupe.

Alifafanua kuwa pamoja na serikali kutoa dawa hiyo, masharti ya kupewa dawa ni kuhakikisha majosho yanafanya kazi na kuna upatikanaji wa maji ya kutosha kwenye majosho na kuanzisha kamati za kuyasimamia.

"Mkikamilisha hayo, tukaja kukagua tukahakiki kuwa mmetimiza vigezo, tunawapatia dawa. Hadi sasa, maosho la Matiani na Eworendeke ndiyo yanafanya kazi, mengine bado," alibainisha.

Alisema kuwapo kwa wadau wa maendeleo wilayani hapa, kumewezeha kukarabatiwa kwa majosho saba kupitia mradi wa Maisha Bora, lakini hadi sasa ni majosho mawili tu ndiyo yanafanya kazi licha ya kukarabatiwa na haelewi tatizo linalokwamisha maeneo mengine.

Aliwataka wafugaji kusimamia mifugo yao kwa umakini na kutoachia mifugo kuzurura kwenye mazingira ya barabara, ili kuepuka kugongwa na hata wakati mwingine kuonekana kero kwenye maeneo ya makazi ya watu ambao hawafugi.

"Punda wameonekana kuzagaa sana Barabara ya Engikaret hadi Namanga, unakutana na kundi lenye punda zaidi ya 200, hawana msimamizi, niombe walindeni na kuwatunza wasionekane kero kwa jamii," aliagiza.

Mfugaji kutoka Kijiji cha Irikaswa Saruni Lukumay alisema, ugonjwa wa vipele umeonekana pia kwa mifugo mingine, hasa mbuzi na kondoo, hivyo akaiomba serikali kutoa chanjo kwa mifugo hiyo pia.

Habari Kubwa