Waziri asisitiza ziara za kushtukiza viwandani

15Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
MKURANGA
Nipashe
Waziri asisitiza ziara za kushtukiza viwandani

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene, amesema ziara za kushtukiza maeneo ya viwanda ni endelevu ili kuhakikisha sheria na taratibu za kuhifadhi mazingira zinafuatwa sambamba na kuhamasisha uwekezaji wa viwanda nchini.

Akizungumza katika ziara yake wilayani Mkuranga katika Mkoa wa Pwani, Simbachawene  alisema serikali inahamasisha na kuvutia uwekezaji katika viwanda kwa kuzingatia sheria na kanuni za utunzaji wa mazingira.

“Kama waziri mwenye dhamana ya mazingira nitaendelea kufanya ziara za kushtukiza sehemu mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa uwekezaji katika viwanda hauathiri mazingira au kuleta adha kwa wananchi sehemu husika,” alisema.

Simbachawene alisema uwekezaji mzuri na endelevu ni ule unaojali na kulinda mazingira yanayozunguka hivyo azma ya serikali ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025 itatekelezwa sambamba na utunzaji wa mazingira.

Kauli ya waziri ilikuja kufuatia ziara ya kushtukiza kwenye kiwanda cha kuzalisha nondo cha Fujian Hexingwang kilichopo eneo la Kisemvule katika Wilaya ya Mkuranga ambapo wananchi walikuwa wakilalamikia kiwanda hicho kwa kutozingatia taratibu za utunzaji wa mazingira.

Simbachawene amewaonya wawekezaji kuacha kutumia mwanya wa ujenzi wa viwanda kwa kukiuka sheria na kanuni za mazingira na kamwe wizara yake haitamvumilia mwekezaji wa aina hiyo.

“Sheria na kanuni zetu za mazingira zinawataka wawekezaji wa viwanda kupitia michakato kadhaa kabla ya kuanza uzalishaji, lakini wapo wawekezaji wanaopita njia za mkato na kuanza uzalishaji, huku miundombinu ya msingi katika viwanda hivyo vikiwa bado havijakamilika hali inayosababisha malalamiko kutoka kwa  wananchi,” alisisitiza Simbachawene.

Aidha, alitoa angalizo kwa viwanda ambavyo vinaendelea na uzalishaji, huku vikiwa vimekamilisha taratibu na sheria za mazingira, lakini wakati uzalishaji ukiendelea viwanda hukiuka taratibu zinazowaongoza.

“Kuna viwanda vimefuata taratibu zote kupitia NEMC, lakini wanapoanza uzalishaji hujikuta wanakiuka taratibu hizo, ofisi yangu kwa kushirikiana na NEMC tutahakikisha tunapitia viwanda hivyo na kama vitabainika kuwa na makosa basi vitapigwa faini kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Simbachawene ameyataja makosa ambayo yamekuwa yakijirudia kwa viwanda vingi ni pamoja na kutiririsha majitaka bila kuyatibu, mfumo mbovu wa utupaji taka za viwandani, hewa chafu na milipuko hali inayochangia uchafuzi wa mazingira na kuleta athari za kiafya kwa wananchi.

“Tunajenga uchumi wa viwanda ambao utaleta uwiano mzuri na ustawi wa jamii, tunawapongeza wale wote ambao wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa kanuni na sheria za mazingira, lakini kwa wale ambao wamekuwa wakikiuka utaratibu basi watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Simbachawene.

Katika ziara hiyo, Simbachawene alikifungia pia Kiwanda cha Fujian Hexingwang kwa kipindi cha mwezi mmoja kwa ukiukwaji wa kanuni za mazingira ambapo  mmiliki wa kiwanda hicho alipewa wa kukamilisha ujenzi wa miundombinu.

Habari Kubwa