Uniti 10,000 zahitajika Tanzania ya viwanda

15Jan 2020
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Uniti 10,000 zahitajika Tanzania ya viwanda

MKURUGENZI wa Shirika la Umeme (Tanesco), Dk. Tito Mwinuka, amesema ili kufikia Tanzania ya viwanda, zinahitajika uniti 10,000 za umeme.

Kutokana na mahitaji hayo, Dk. Mwinuka amesema Tanesco imejipanga kimkakati ili kufanikisha azma hiyo ya serikali.

Aliyasema hayo jana alipofungua mafunzo elekezi kwa baadhi ya wafanyakazi wapya wa shirika hilo, akibainisha kuwa liliajiri watumishi wapya 958 hivi karibuni.

“Tanesco tumejipanga vilivyo kushiriki katika miradi ya serikali ili Tanzania ya viwanda ifikiwe na pia kutoa huduma ya umeme kwa wawekezaji na wananchi kwa ujumla," alitamba na kuongeza:

"Kuelekea Tanzania ya viwanda, tunahitaji kufikia uniti 10,000, hivyo ni vyema mikakati yetu tuiweke sawa ili tufikie malengo tuliojiwekea."

Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dk. Emmanuel Shindika, aliwataka wafanyakazi hao wapya kuhakikisha wanasimamia maadili waliyofundishwa ili kufanya kazi kwa uadilifu.

Alisema hakuna sababu ya kupindisha sheria zilizowekwa kazini, badala yake kuzifuata kama maadili ya utumishi wa umma yanavyoelekeza.

"Nawaomba zingatieni yale mliofundishwa, hakuna sababu ya kufanya kinyume cha maadili elekezi ya kazi, "alishauri.

Alisema wamefundishwa kila walichostahili kufanyiwa na mamlaka husika hivyo nao wanapaswa kutendea haki na si kubweteka.

Wafanyakazi wamepewa mafunzo elekezi ya siku sita kabla ya kuanza kazi ili kwenda sambamba na kasi ya shirika hilo katika utendaji wao.

Habari Kubwa