Wavuvi Mafia wataka mafunzo sheria, kanuni

15Jan 2020
Beatrice Philemon
Nipashe
Wavuvi Mafia wataka mafunzo sheria, kanuni

WAVUVI katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Mkoa wa Pwani wameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwapa mafunzo juu ya sheria na kanuni za uvuvi ili kufahamu kitu gani kinatakiwa katika sekta ya uvuvi na kunufaika na shughuli za uvuvi.

Akizungumza kwa niaba ya wavuvi, Katibu wa Chama cha Ushirika Twendekazi Mibulani, Twaha Ismail, alisema kuwa wanaiomba serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuwapa mafunzo kwa sababu hivi sasa vijana wengi wanaomaliza darasa la saba wanajikita katika shughuli za uvuvi na wengi wao hawajui sheria za uvuvi.

Alisema ingawa vijana hao wana leseni za uvuvi kutoka halmashauri, lakini wengi wao hawajui  sheria za uvuvi…wanajivulia tu na mwisho wake wanakuja kukamatwa na maofisa uvuvi.

"Tunaomba watu wa idara ya uvuvi waje kutoa mafunzo kwa wavuvi kuhusu sheria za uvuvi na siyo kuja kukamata watu tu, na mvuvi akivunja  sheria hizo ndiyo akamatwe," alisema.

Alisema hivi sasa katika Wilaya ya Mafia kuna watoto wengi wa darasa la saba wanataka kuingia kwenye sekta ya uvuvi, lakini hawajui sheria za uvuvi.

Pia waliiomba wizara kuwawezesha wavuvi kuwa na vyombo vya kisasa ili waweze kwenda kwenye kina kirefu kuvua samaki.

Alisema wakazi wa Mafia  hawawezi kuondokana na umaskini bila kuwa na vyombo vya kisasa.

“Asilimia kubwa ya wananchi wa Mafia, wanatumia  mitumbwi midogo ambayo haiwezi kwenda mbali kuvua samaki  wala kupata samaki wengi, alisema.

Wavuvi hao walisema kuwa ingawa ActionAid Tanzania wamewawezesha  kupata elimu ya masuala mbalimbali ikiwamo kupewa boti ya kisasa, wanaiomba pia Halmashauri ya Wilaya ya Mafia iwawezeshe kupata elimu ya uvuvi  kutoka kwa wataalamu  wa Chuo cha Uvuvi Mbegani ili kufanya shughuli za uvuvi kisasa.

“Tunaomba halmashauri  yetu  itusaidie katika suala hili kwa sababu uvuvi tunaovua ni wa asili ambao umepitwa na wakati, tunatumia mitumbwi midogo midogo  ambayo haiwezi kwenda  mbali na kuwasaidia kuvua samaki wengi,” alibainisha.

Vilevile wanaiomba halmashauri iwawezeshe nyenzo za uvuvi za kisasa, na kuwa wako tayari kukopeshwa kwa sababu wanafanya kazi katika mazingira magumu, ambayo ni hatarishi kwa maisha yao na  kipato chao hakiongezeki.

Naye Ofisa  Uvuvi wa Wilaya, Ayoub Sabu, alisema kazi ya halmashauri ni shughuli zote zinazohusiana na uvuvi endelevu, kutoa vibali maalumu vya shughuli za uvuvi, kufuga na kuvua,  kutoa elimu kwa wavuvi juu ya uvuvi endelevu na kutunza viumbe maji (mwani).

Pia shughuli nyingine kubwa wanazozifanya ni kuunganisha wavuvi, wafanyabiashara kujiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka.

Kwa sasa wizara ina mkakati wa kusaidia wavuvi kukopesheka hasa vikundi vidogo vidogo na vyama vya ushirika na pia mpaka sasa halmashauri imeunda vikundi viwili vya wavuvi katika eneo la Kilindoni.

"Mara nyingi tumeshindwa kutoa mafunzo kwa wavuvi kutokana na uhaba wa watumishi wa sekta ya uvuvi na uhaba wa bajeti ili kufikia watu hao," alisema

Wilaya ya Mafia ina wavuvi 5,133 na vyombo vya uvuvi 1,011 ikiwamo mitumbwi, boti na ngao.

Habari Kubwa