Katwila afurahia rekodi Mtibwa ikitwaa Kombe

15Jan 2020
Isaac Kijoti
ZANZIBAR
Nipashe
Katwila afurahia rekodi Mtibwa ikitwaa Kombe

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, ameeleza kufurahia kuandika rekodi ya kulitwaa Kombe la Mapinduzi akiwa mchezaji na sasa kocha wa timu hiyo.

Mtibwa Sugar juzi usiku ilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Simba bao 1-0 kwenye mechi ya fainali iliyopigwa Uwanja wa Amaan visiwani hapa.

Bao pekee katika mechi hiyo ambayo Simba ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, lilifungwa na Awadh Salum katika dakika ya 38 akipokea pasi kutoka kwa Jaffar Kibaya.

Hiyo ni mara ya pili kwa Mtibwa Sugar kutwaa ubingwa huo baada ya kuutwaa mwaka 2010 kwa kuifunga Ocean View katika mchezo wa fainali wakati huo Katwila akiwa mchezaji wa 'Wanatamtam' hao.

Akizungumza na Nipashe baada ya mechi hiyo, Katwila alisema ni furaha kwake kuweka rekodi hiyo Mtibwa kwa kuifunga timu bora kama Simba.

"Nilitwaa ubingwa huu nikiwa mchezaji na timu hii ya Mtibwa na leo nimelitwaa tena kombe hili nikiwa kocha wa timu hii, najisikia furaha sana kwa rekodi hii," alisema.

Alisema ilikuwa fainali ngumu hasa kwa kuwa alikutana na timu bora ambayo inaundwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa juu.

"Simba ni timu bora na ndiyo inayoongoza Ligi Kuu Bara, hivyo kwanza tuliiheshimu kwa hilo, lakini tulipambana na kupata ushindi, nawapongeza sana wachezaji wangu kwa kufuata maelekezo niliyowapa," alisema.

Kwa ubingwa huo Mtibwa imelamba Sh. milioni 15, kombe na medali za dhahabu wakati Simba ikiambulia Sh. milioni 10 na medali za fedha.

Habari Kubwa