Serikali Zanzibar yampongeza Kiba

15Jan 2020
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Serikali Zanzibar yampongeza Kiba

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewataka wasanii kutambua jukumu lao ndani ya jamii la kuelimisha kwa kutumia sanaa ili kusaidia maendeleo na mabadiliko muhimu ya taifa.

Balozi Iddi alisema licha ya sanaa kuchukua nafasi kubwa katika kutoa burudani na ujumbe wake kuifikia jamii kirahisi, lakini bado anaamini haijatumika vema.

Kiongozi huyo alisema hayo jana ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Msanii maarufu wa bongo flaca nchini, Ali Kiba aliyepo visiwani hapa kwa ajili ya kusaidia jamii katika kampeni yake ya Ali Kiba ‘Unforgettable’.

“Itapendeza zaidi kama jamii itaendelea kushuhudia sana, inatumiwa vyema katika kuelimisha kwa vile ni moja ya sehemu inayoweza kufundisha kwa urahisi,”alisema Balozi Iddi.

Alisema wasanii wengi wa kikazi kipya wanajishughulisha na nyimbo zinazokiuka maadili hasa mavazi jambo ambalo ni hatari kuigwa na watoto ambao ni Taifa la baadae.

Kiongozi huyo alimpongeza na kumshukuru msanii huyo kwa kampeni yake ya kusaidia jamii kupitia mapato yake na kumwahidi kumpa ushirikiano zaidi katika kazi hiyo anayoifanya.

Kwa upande wake, Kiba alisema aliamua kuunda kampeni hiyo kwa lengo la kuondoa dhana iliyojengeka kwa baadhi ya watu kufikiria kwamba muziki ni sehemu ya uhuni.

Kiba alisema muziki hutoa ajira nyingi kwa kundi kubwa la vijana walioamua kuendesha maisha yao kupitia sanaa hiyo na ndani yake kuna ujasiriamali.

Kuhusu kampeni hiyo, alisema inalenga kutoa huduma za Afya katika upimaji bure pia huwatembelea wanafunzi wa vyuo vikuu, ili kuwajengea uwezo wa kutumia vyema elimu wanayoipata.

Habari Kubwa